The House of Favourite Newspapers

Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani-19

1

ILIPOISHIA:

 

Aliondoka na kuelekea upande wa vyumba ilionekana anakwenda kutandika kwenye chumba cha Papaa kama jina lake nilivyolisikia. Sikutaka kujihoji tena kwa vile niliamini ule haukuwa muda wake huenda kina Doi walikuwa wakijua kila kitu juu ya biashara ile.

Kilichonishangaza  shoga zangu kuondoka na kuniacha huku wakijua mimi mgeni japokuwa walinieleza popote nitakapokuwepo siwezi kupotea kurudi nyumbani.

 

SASA ENDELEA…

 

Nilichukua glasi ya bia na kugida funda kadhaa na kuteremsha chini. Nilikuwa nimetulia kama mtawa kweli lakini nilikuwa napiga ulabu. Nilikumbuka usiku nilipokuwa nazungumza na Papaa kuwa anataka kufanya biashara na mimi yenye malipo mazuri pengine itasababisha kuachana na kazi ya ukahaba.

Lakini bado nilijiuliza pale ni wapi na wale akina nani na wanafanya kazi gani, mazingira yalionesha kama ni makazi ya kidini, lakini nilibaki na swali na kujiuliza kama ni watumishi wa Mungu mbona ni malaya wanaotenda dhambi.

Lakini bado niliamini majibu ya maswali yangu yatajibiwa na shoga zangu, nikiwa naendelea kukata ulabu yule dada alikuja na simu ambayo ilikuwa bado ipo hewani na kuniambia:

“Zungumza na mkuu,” nilichukua simu na kuzungumza:

“Haloo.”

“Eeh! Murembo.”

“Ndiyo Papaa,” nilijua ni yeye baada ya kusikia lafudhi yake.

“Sasa ni hivi, samahani nilitoka bila kukuaga, kuna mutu nitamtuma atakuletea pesa yako. Najua itakutosha hata tungepatana isingefikia pesa hiyo ni nyingi sana.”

“Asante.”

“Una simu?”

“Sina.”

“Mutu atakayekufuata atakuletea simu mupya ya kisasa ina laini kabisa wewe ni kutumia salio halitaisha leo wala kesho.”

“Asante Papaa.”

“Kama tulivyozungumza jana, jioni nitamtuma mutu akufuate ili tuje tuzungumze jinsi ya kuifanya biashara yetu.”

“Sawa Papaa.”

“Basi nikuache tuonane jioni, kwa sasa naomba uachane na biashara ya mwili utadili na mimi, sawa murembo?”

“Hakuna tatizo.”

Baada ya kuzungumza Papaa nilimrudishia dada simu yake naye aliendelea na kazi zake. Baada ya muda kengele ililia, dada alitoka chumbani na kwenda kufungua mlango. Kabla ya kufungua alinieleza nimsaidie kupokea wageni na kuwahudumia kifungua kinywa mpaka watakapoondoka walikuwa hawakai sana, nilimkubalia.

Kabla ya kufungua mlango aliondoa glasi ya bia kisha aliwafungulia waliingia wageni sita, Wazungu wanne na Waswahili wawili. Wote walikuwa wamevaa kichungaji, walitusalimia kwa jina la Bwana.

“Bwana Yesu asifiwe.”

“Amen,” niliitikia huku nikipeana nao mikono kwa kupiga magoti kwa heshima kitu kilichokuwa tofauti na mwenzangu.

Tuliwakaribisha katika chumba kingine kilichokuwa kimeandalia kifungua kinywa, nilishirikiana na yule dada kuwakaribisha wageni kwa unyenyekevu mkubwa. Ilikuwa tofauti na alivyofikiria mwenzangu labda nitakosea, lakini nilipita mlemle kwa vile hakukuwa na kitu kigeni pia niliujua usanii kisawasawa bila usanii kazi yetu haiendi.

Ilikuwa ajabu baada ya kupata kifungua kinywa, mmoja wa wachungaji Mzungu alinipa zawadi ya pesa kutokana na kupendezwa na huduma yangu. Baada ya kuondoka mdada alinishangaa na kusema:

“Dada wewe kiboko.”

“Kwa nini?”

“Yaani umenishinda hata mimi mwenye kazi yangu.”

“Walaa, mimi nilikuwa nakufuatilia ili nisiharibu,” nilimpa kichwa.

“Basi umenifurahisha sana, nitakutafuta nataka uwe shoga yangu.”

“Hakuna tatizo.”

Baada ya saa moja tangu wageni watoke alifika kijana mmoja mtanashati na kusema:

“Dada jiandae tuondoke.”

Nilikwenda kubadili nguo na kuagana na shoga yangu kwa kuniandikia namba yake ya simu kwenye karatasi. Nilikwenda kuingia kwenye gari ili kurudishwa nyumbani Kawangware. Tulipofika yule kaka alinipa pesa yangu iliyokuwa kwenye bahasha na simu ya gharama.

“Mzigo wako huu.”

“Asante,” nilipokea.

 Niliteremka kwenye gari na kuagana na dereva, nilichepua mwendo kuingia ndani sikupenda watu wanishangae na vazi langu tata nililovaa. Shoga zangu walishtuka kuniona huku Doi akiamka na kunikumbatia kwa furaha.

“Waaaooo Konso.”

“Jamaniiii.”

“He! Shoga kulikoni?” Doi aliniuliza akiwa kama anishangaa.

“Mmh! Temea mate chini mtasema nina kizizi, nimetengeneza pesa ya mwezi kwa siku moja.”

“Achaa.”

“Nani ana simu ya gharama kama mimi?” niliwaonesha simu yangu.

“Haa! Jamani,” wote walishika midomo yao.

“Mbona mnashtuka?”

“Yaani leoleo tu umetushinda wenyeji wako.”

“Kila mtu na bahati yake, wengine tulipozaliwa tumeoshewa na majani  mfedhafedha hivyo msishangae fedha kutufuata.”

“Mmh! Umetisha hebu tupe siri ya ushindi?”

“Kwa kweli ninyi ndiye wenyeji wangu, ndani tumeingia wote na kilichondelea mlikiona, yule mkaka sijui Jose aliyeambiwa anipeleke chumbani wakati akinipeleka alikuwa akilalamika kuwa kachukuliwa mzigo wake.”

“Mzigo wake upi?”

“Yaani mimi, kumbe alijua analala na mimi lakini bosi wao katumia madaraka kunimiliki mimi.”

“Na kweli jana ilikuwa ajabu, yule bosi wao huwa hashughuliki na sisi…”

Je, nini kitaendelea? Usikose siku ya Jumatano.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

1 Comment
  1. Ahady kidehele says

    Laaaana za ulimwenguuu

Leave A Reply