The House of Favourite Newspapers

Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani-5

0

ILIPOISHIA:

Baada ya kusafishiwa gari niliongozana na Bantu kuelekea nyumbani kwangu. Moyoni niliona kwa mtindo ule siwezi kuwekewa mipaka hata kama nitakuwa na mwanaume wa nje hawezi kunizuia.

Tukiwa njiani nilimuuliza maswali mawili matatu juu ya maisha yake
“Bantu ina maana hii ndiyo kazi yako ya kila siku?”

SASA ENDELEA…

“Ndiyo sister, hizi kazi za kuajiriwa zinakwenda kwa majina bila kuwa na refalii cheti chako utafungia maandazi.”
“Unajua kuendesha gari?”
“Ndiyo.”

“Umejifunzia wapi?”
“Hapahapa, kila tukimaliza kuosha tunawageuzia magari yao.”
“Umesoma?”
“Ndiyo.”

“Mpaka darasa la ngapi?”
“Kidato cha sita.”
“Muongo!” Sikumuamini kuona kijana mwenye elimu kama yake anaosha magari.
“Kweli kama nilivyokueleza bila refa hakuna kinachoendelea.”
“Una vuta sigara?”
“Hapana.”

“Pombe unatumia?”
“Hapana..mimi starehe yangu mpira jioni hujichanganya kwenye mazoezi.”
Tulipofika nyumbani nilimpeleka hadi sebuleni, cha kwanza nilimpeleka bafuni kuoga kisha nilimpa nguo ambazo aliziacha yule kijana aliyenitapeli mwanzo. Nilimweleza madhumuni ya kumpeleka, nilishukuru kijana wa watu alinielewa.

Niliamua kuyabadili maisha ya Bantu, kwa muda mfupi Bantu alipendeza kweli nguo humfanya mtu aonekane duni au aonekane kiumbe kipya machoni mwa watu, nilimpa kila kitu nilimnunulia vitu vya thamani na kuonekana kijana wa kileo anayeendana na mimi..

Tangu hapo tukawa tupo pamoja mimi na Bantu popote alipokwenda, pamoja na kuwa na Bantu lakini nilikuwa na wazee wenzangu ambao nilifanya nao starehe kwa nafasi kwa kujua Bantu nilimpa mipaka yake.

Taarifa za Bantu kuwa na uhusiano na mmoja wa wafanyakazi wangu wa saluni, yalininyima raha japo hata mimi sikuwa muaminifu kwake lakini yeye nilikuwa kama nimemuoa nampa kila kitu alichotaka.

Nilimueleza ukweli Bantu kama atafanya upuuzi wake nitamrudisha kijiweni kwake. Bantu alisema kuwa hayo ni maneno ya uzushi kwa kuwa nilikuwa nampenda nilimkubalia.

Siku moja nikiwa kwenye moja ya saluni zangu nilipigiwa simu na mtu nisiyemjua na kunieleza kuwa Bantu ameonekana sehemu na mmoja wa wafanyakazi wangu na kunielekeza niende sehemu ile.

“Haloo,” ilikuwa sauti ya kike.
“Haloo, nani mwenzangu?”
“Si lazima kujua jina langu, nenda Furaha Hoteli chumba namba 122.”
“Nikafanye nini?”

“Mfanyakazi wako anakuzunguka kwa mpenzio Bantu.”
“Wee nani?” sikujibiwa zaidi ya simu kukatwa.
Niliondoka nikiwa nimechanganyikiwa kwenda sehemu niliyoelekezwa na kuiona hiyo hoteli. Niliingia na kwenda moja kwa moja hadi chumba nilichoelekezwa. Niligonga baada ya muda mlango ulifunguliwa, nilikutana uso kwa uso na mfanyakazi wangu akiwa kwenye taulo bila kitu chochote mwilini, ilionesha si muda mrefu walimaliza kufanya uchafu wao.

Aliponiona alishtuka nusra azirai kwa mshtuko, nilimsukuma ndani na kuingia kama polisi. Nilimkuta Bantu akiwa amejifunika shuka mwisho kiunoni kifua kilikuwa wazi na nguo zake zilikuwa juu ya kochi.

“Ha! Bantu unafanya nini?”
Bantu alishtuka na kujikuta akinyanyuka bila kujielewa na kubakia mtupu na kuja kuniomba msamaha. Kwa hasira nilimuuliza huku nikilia:
“Bantu nilikwambia nini umerudia nini?”

“Nisamehe anti Konso,” Bantu alipiga magoti mbele yangu akiwa mtupu kama mwanga.
“Bantu huna tofauti na jini lililotolewa kwenye chupa ambalo baada ya kushukuru linataka kukumeza, huna budi kurudishwa kwenye chupa kijiweni kwako,” nilisema kwa hasira.

“Hapana anti Konso ni shetani tu kanipitia, ukiniacha nitakuwa mgeni wa nani?” Bantu alizidi kunibembeleza huku msichana wangu wa saluni akiwa amejikunyata kwa woga.
“Utajijua nipe funguo za gari langu,” nilikwenda hadi kwenye suruali ya Bantu na kuchukua funguo za gari langu kisha niliondoka kwa ghadhabu nikiwa nimevimba kama nataka kupasuka.

Nikiwa njiani niliwaza mengi juu ya tukio nililoliona muda mfupi, nilijiuliza nini anachokikosa kwangu mpaka aamue kutoka nje tena na mfanyakazi wangu wa saluni. Nilijiuliza nina upungufu gani ambao sikuujua, mbona wanaume wananiganda kama luba na kutangaza ndoa wanapo nionja tu au Bantu amenikinai, mbona mapema au kuna kidudu mtu anayetaka kunihujumu!

Sikuwa na haja ya kwenda saluni, nilirudi nyumbani moja kwa moja na breki ya kwanza ilikuwa kwenye jokofu, nikachukua pombe kali na kumimina katika glasi na kunywa. Siyo siri japo nimemfukuza Bantu nilikuwa bado nampenda kwa vile alikuwa na sifa za mwanaume anayependeza kuwa naye.

Nilimimina glasi nzima iliyokuwa imejaa mvinyo mkali kwenye mdomo kisha nikameza kwa kukunja uso, nilijaza nyingine ambayo nilikunywa taratibu huku machozi yakinitoka, nilikumbuka nilivyo mfumania Bantu.

Pamoja na ujasiri wangu wa kutobabaikia wanaume, kitendo cha Bantu kiliniuma sana, hasa ukizingatia alitakiwa anishukuru kumtoa kwenye maisha mabaya, kweli mbuzi kamba ni yake mnyororo unamuonea pia mfadhili mbuzi utamfaidi hata mchuzi lakini binadamu utaambulia maudhi.

Nikiwa bado naendelea kunywa pombe kwa fujo, Bantu aliingia na kuja kunipigia magoti mbele yangu kuniomba msamaha.
“Anti Konso naomba unisamehe sirudii tena.”
“Bantu au kwa vile nimeonesha nakupenda ndiyo umeamua kunifanyia upuuzi kama ule?” nilimuuliza huku nikiendelea kulia.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Jumatano, siku ya Jumatano.

Leave A Reply