The House of Favourite Newspapers

Nilivyoteseka Kwenye Mianzi ya Kichawi- 11

0

ILIPOISHIA

…tutafia kwenye shimo hilo kama walivyokuwa hao ambao mifupa yao sasa tunaitumia kama vifaa vya kuchimbia njia yetu ya kujinasua.

SASA ENDELEA
Mwongozo wetu kama nilivyosema awali ni njia ya panya ambayo kwa bahati nzuri ilikuwa siyo ya kupindapinda.

Kazi hiyo tuliifanya kwa siku mbili mfululizo, mchana.
Ilikuwa kazi kubwa kwa sababu kwenye tundu tulilokuwa tunalichimba kulikuwa na giza na joto sana.
“Inabidi tuingie kwa zamu kwenye hili tundu tunalolichimba,” nilishauri.
Kilichosaidia ni kwamba ndani ya shimo hilo la kifo kulikuwa na upana wa kutosha na tulitumia nafasi fulani kulundika mchanga unaotolewa kwenye tundu.
Hata hivyo, kuliongezeka joto ndani ya shimo kutokana na kupungua nafasi baada ya sehemu nyingi kumezwa na mchanga uliokuwa ukisomwa kwa mafuvu ya watu.
Changamoto nyingine ambayo tulikumbana nayo ni ya kuuguliwa kwa mwenzetu mmoja wa kike.
“Kaka mimi najisikia kuumwa,” alisema msichana huyo.
“Unaumwa nini?”
“Naumwa sana na tumbo na mwili wote najisikia homa,” alisema.
Nilikwenda kumgusa kwa kutumia kiganja change nikakuta kweli ana homa kali. Niliogopa japokuwa sikutaka wenzangu waone kuwa nina woga.
Woga huo uliniingia kwa sababu kuu mbili. Moja, nilihofu kwamba kama ni malaria anaweza kufa.
Pili nilijua kwamba akifa tukiwa kwenye pango lile ambalo lilikuwa na joto kali, ataharibika, hali itakayosababisha kuwe na harufu kali na kwa vyovyote watu wataishiwa nguvu ya kufanya kazi, hivyo wote kufia kwenye shimo hilo la kifo.
“Jamani huyu anayeumwa akandwe kwa maji, haya wasichana fanyeni kazi hiyo,” niliamuru.
Bila ajizi wasichana wakawa wanamkanda mwenzo mgonjwa kwa kutumia khanga zao.
“Angalieni, mtumie maji kwa uangalifu kwa sababu hatuna maji zaidi ya hayo,” niliwaonya.
Nilihesabau chupa za maji ambayo yalibaki zilikuwa kama kumi na tano tu. Niliogopa sana.
Mikate tuliyopewa na wale watu ili ikiisha tufe kwa njaa ilikuwa mingi kuliko maji.
Lakini nilijua kuwa kama maji yatakwisha hata kama tuna mikate mia moja, tutailaje? Kwa vyovyote tutashindwa.
Wakati tunajitahidi kuchimba mtaro huo ili tuweze kutoka nje kijana mmoja aliyekuwa ndani aliniita:
“Kaka Namakoto, kaka namakoto njoo upesiii!”
Nikajikusanya kutoka katika kundi la yule msichana mgonjwa na kuinama ili kwenda ndani ya tundu ilikotokea sauti.
“Kaka Namakoto njooo,” alisema kijana mwingine, staili ya uitaji wao ilinitia wasiwasi na kunifanya nijiulize mara mbili, hao wameona mwanga au kitu gani kimewafanya wapagawe!
Nilikuwa na kibiriti mkononi, nikakiwasha baada ya kuwafikia.
“Nini?”
“Kuna majimaji hapa,” mmoja alisema.
Niliwasha kibiriti na kugundua kuwa kweli kulikuwa na unyevunyevu.
Tulizidi kuchimba sasa badala ya kutia mchanga kwenye mafuvu ya kichwa tukawa tunatia tope yaani mchanganyiko wa maji na udongo.
Wakati wenzangu walikuwa wakifurahia hali ile, akili yangu haikukaa sawa, nilihofu kwamba kutokana na majimaji yale tunaweza kufunikwa na udongo.
Vijana walikuwa wakiendelea kuchimbua licha ya mikono yao kuwa na malengelenge kutokana na kutozoea kazi za sulubu walizokuwa wakifanya.
“Ngojeni kidogo, kuna kitu nimewaza,” nilisema.
“Umewaza nini tena? Tujitahidi jamani tunaweza kuibuka juu ya ardhi,” alisema Kwimuka.
“Hapana. Akili hainitumi kuendelea mbele.”
“He, kaka Namakoto ina maana tuache, kisha iweje?” aliuliza tena Kwimuka.
“Simahanishi kwamba tuache kazi ya kuchimba hapana.”
“Ila?”
“Tumchimbe sasa kuelekea juu, si mnaona jinsi kulivyojaa tope hapa chini?”
“Ndiyo.”
“Mnajua kwa nini nasema hivyo?”
“Hatujui.”
“Tuelekee juu kwa sababu tukiendelea mbele kuna hatari ya hili tundu kutufunika.”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Nimeshasema tuchimbe kwenda juu ili kama kutokeza basi tutokeze juu ya ardhi.”
“Kuna mwenye wazo zaidi ya langu?”
“Hakuna,” alijibu haraka haraka Kwimuka.
“Hapana, haya mambo siyo ya mtu mmoja, inafaa kila mmoja akatafakari kabla ya kujibu,” nikawapa wosia.
Baada ya kukaa kwa sekunde karibu kumi bila kupata jibu mmbadala, tukaanza kazi ya kuchimba kwenda juu.
Kasi hiyo ilikuwa nyepesi kidogo kwa sababu kila ukichimbua ardhi ilikuwa inaanguka kutokana na kulowana na maji.
Usiku ulipoingia tulitengeneza kama kisima ili kukinga maji ambayo yangeweza kutusaidia ikiwa tutaishiwa kabisa maji.
Kulipopambazuka nilikwenda kuona kama maji yamepatikana, nikawasha kibiriti na kukuta yamejaa ya yamejikusanya kwenye shimo tulilolitengeneza maalum kwa ajili ya kazi hiyo.
Niliwaambia wenzangu wachukua chupa zote tupu na wajaze maji yale ili yatusaidie siku zijazo.
Wakati huo hali ya mgonjwa wetu ilizidi kuwa mbaya na hatukuwa na dawa yoyote ya kumpa sipokuwa maji.
Wakati natia maji kwenye chumba niliona mzizi fulani ambayo ilinipa ishara kwamba tunakaribia kutoboa juu ya ardhi.
Rangi ya mzizi hiyo ilinikumbusha zamani wakati nikiwa na marehemu babu yangu ambaye alikuwa na kawaida ya kunionesha mizizi mbalimbali ambayo alikuwa akiitumia kutibu watu.
“Huu mzizi kama wa mti mmoja unaitwa Nrokochi. Babu alikuwa akiutumia kutibu maradhi mbalimbali.”
“Una uhakika?” alinihoji kijana mmoja.
“Ngoja kwanza tuufuatilie.” Tulichimba kuufuata na baadaye kuukata.
Je, watafanikiwa kujiokoa? Fuatilia MWISHO Jumanne ijayo.

Leave A Reply