The House of Favourite Newspapers

Nilivyoteseka Kwenye Mianzi ya Kichawi – 5

0

ILIPOISHIA 

Wakati yote hayo yanafanyika mimi nilikuwa bado nimepigishwa magoni na kwa hakika magoti yalianza kuniuma kwa sababu pale chini palikuwa na changarawe na sikuthubutu kusimama au kukaa kwani niliwaza kwamba nikifanya hivyo, watanimaliza kwa mikuki yao.

SONGA NAYO…

Niliwaza hivyo kwa sababu nilijua kuwa kilichotufikisha pale ni kutotii sheria za kwenye bustani ya mianzi ya          Nangose , sasa kutotii sheria mbele ya mfalme nilijiridhisha kuwa adhabu yake itakuwa kali na ya papo kwa hapo, yaani ama nikatwe kwa panga shingoni au kukitwa mkuki kifuani au mgongoni na kufa palepale.

Baadaye ngoma zilizokuwa zikipigwa zilisimama na nikamuona mfalme au chifu wa mji ule akishuka jukwaani alipokuwa huku akiwa bado ana panga mkononi. Nilihisi moyo kuchomoka kwa jinsi ulivyokuwa ukidunda kwani nilijua kuwa sasa anakuja kunikata kichwa.

Lakini nilijisemea moyoni kwamba akija kwa kusudio hilo sitakubali kuuawa kinyonge, kwamba ni lazima nitapambana naye. Nilijisemea hivyo kwa sababu hadi chifu au mfalme huyo anashuka, sikuwa nimefungwa mikono wala miguu, hivyo ningeweza kujitetea japokuwa nilijua kuwa kifo sitaweza kukiepuka kwa sababu wale watu wapo wengi na wanaume karibu wote walikuwa na mikuki.

Niliwaona wale wanawake kumi na mbili waliokuwa wakicheza wakiwa na mitungi kichwani, wakiitua na kuiweka mbele yangu.

Mfalme badala ya kunijia mimi aliiendea ile mitungi na kuteka maji kisha kumpa yule mzee Mavaka tuliyemkuta katika bustani ya Nangose aliyekuwa amesimama karibu yangu.

Wazo lingine lilikuja na kujiuliza hawa jamaa wanataka kuniua kwa kuninywesha maji yaliyokuwa kwenye mitungi yote kumi na mbili? Sikupata jibu.

Badala yake yule mzee Mavaka alichukua kata iliyokuwa na maji aliyokabidhiwa na mfalme na kupanda jukwaani ambapo kulikuwa kumelazwa wale wasichana wawili tuliokuwanao waliokuwa wamezimia na akaanza kuwamwagia mwilini.

Wa kwanza alipomwagiwa, alizinduka na akakaa palepale juu jukwaani. Msichana wa pili ilitumika mitungi zaidi ya mitatu kumwagiwa mpaka nikawa na wasiwasi kwamba inawezekana ameshakata roho.

Wakati nakata tamaa, mara nilisikia akikohoa, hapo moyo wangu ukatulia, nikaona Mungu amemponya. Wakati hayo yanafanyika, uwanja mzima ulikuwa kimya na aliyekuwa akitembea      huku akiwa na kata yenye maji na akiwa anafanya kazi ya kuwamwagia maji wale wasichana ni mzee Mavaka tu.

Baada ya wale mabinti kuzinduka, mfalme alimuita mzee Mavaka na kumuuliza kama yupo tayari kuyasema makosa yetu sisi watu ishirini na sita.

“Ndiyo mfalme, nipo tayari kueleza makosa yao,” akasema mzee Mavaka.

“Eleza sasa,” mfalme akaamuru.

“Hawa vijana walikuja katika bustani yetu ya Nangose na kupata maelezo yote kuhusu masharti. Ajabu ni kwamba walikuwa wabishi na wajeuri. Wakaanza kuchuma matunda na maua na kukata mianzi bila ruhusa tena ile michanga.”

 “Kha! Walikata mianzi michanga kweli?”

“Kweli mfalme na ndiyo maana nimewaleta hapa mbele yako.”

“Uliwaambia adhabu ya kukata mianzi michanga?”

“Sikuwaambia, lakini niliwaambia ni marufuku kufanya hivyo.”

“Baada ya kula matunda na kuchuma maua kisha kukata mianzi ulichukua hatua gani?”

“Hatua ya kwanza ilikuwa ni kuwafokea ili waone kile walichokifanya ni kitu kibaya lakini kwa kuwa kukata mianzi michanga hukumu yake unaitoa wewe, niliona ni vema kuwaleta kwako na ndiyo maana wako mbele yako sasa hivi.”

“Sawa, huyu aliyepiga magoti ni nani?”

“Walijitambulisha kwangu kuwa huyu ni kiongozi wao, anaitwa Issa Namakoto.”

“Bwana Namakoto, umesikia mashtaka yenu?”

“Mheshimiwa mfalme nimesikia, lakini nakuomba sana tusamehe, hatutarudia tena.”

“Hakuna cha kusamehewa. Kuna sheria hapa na sheria ni msumeno. Adhabu yake wote nyinyi ni kifo.”

Mfalme baada ya kusema hayo wenzangu wote wakaangua kilio, isipokuwa mimi. Nilikuwa nafikiria njia ya kujiokoa na kuwaokoa wenzangu.

“Mfalme nimesikia ulichokisema kwamba tunastahili kufa. Nakuomba sana, mimi kiongozi wao ni mtume wa Mungu, nakuomba sana tuepushie na adhabu yako mtukufu na utaona faida yake!” Nilisema kwa ujasiri huku nikijua kuwa nadanganya, sikuwa mtume.

“Nyinyi ni lazima mfe ili iwe fundisho kwa watu wanaofanya vitendo kama vyenu.”

“Tafadhali mfalme…” alinikatiza.

“Nisikilize. Adhabu yenu itakuwa ni kutumbukizwa kwenye shimo refu na humo kila mmoja wenu atajifia kwa wakati wake.”

“Lakini mfalme, ungetusikiliza kwanza…”

“Hakuna cha kuwasikiliza. Wote mtatupwa kwenye shimo refu, hiyo adhabu itaanza kutekelezwa kesho.”

Mwili wangu ulianza kutetemeka tena maana sikujua hilo shimo litachimbwa saa ngapi na sisi kufukiwa kesho au lilishachimbwa tayari.

Baada ya maneno yale ya mfalme, ngoma zilianza kupigwa tena na wale wanaume wenye mikuki wakaanza kucheza kwa kurukaruka kama Wamasai waliopandwa mori.

Wale wasichana wawili waliokuwa juu ya jukwaa waliozinduka walishushwa na wanawake wenzao na kuunganishwa na wengine wakaambiwa wawafuate wale wasichana kumi na mbili waliokuwa na mitungi.

Sisi wavulana tuliambiwa tuwafuate wale wanaume wenye mikuki. Nilijua hakutakuwa na mauaji tena ya kutumia mikuki kwa kuwa adhabu yetu ilishatangazwa kuwa ni kutupwa kwenye shimo siku iliyofuata.

Wavulana tulipelekwa kwenye nyumba moja ndefu kama ‘godauni’. Tuliketishwa chini mle ndani na baada ya muda kikaletwa chakula, kilikuwa chakula kingi na ni tofauti, tuliambiwa tuchague. Kulikuwa na pilau, wali mweupe na nyama.

Zile nyama zilikuwa za aina mbalimbali, zipo tulizoambiwa ni za ng’ombe, ngamia, mbuzi, kuku na bata. Mimi niliamua kujipakulia wali na nyama ya kuku.

Hata hivyo, hakuna aliyekuwa na hamu ya kula kwa kuwa tulijua kesho yake tungeuawa.

Je,nini kitaendelea? Fuatilia Jumanne ijayo. 

Leave A Reply