The House of Favourite Newspapers

Nimeikalisha Familia ya Matumla, Mmalawi Atakaa Tu

0

Chichi Mawe akisaini mkataba wa pambano hilo mbele ya Yassin Abdallah ‘Ustaadh’

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ ni moja kati mabondia bora katika mchezo huo hapa nchini kutokana na heshima na rekodi kubwa aliyojiwekea. Chichi Mawe ambaye amecheza jumla ya mapambano 62, ameshinda 41, 24 yakiwa ni KO, amepoteza 17 kati ya hayo 14 ni kwa KO pia na ametosa sare mapambano manne huku pambano lake la kwanza akicheza mwaka 1998.

Chichi Mawe ni miongoni mwa wanamasumbwi watatu wa Tanzania akiwemo Nasib Ramadhani ‘Pac Man’ na Idd Pialali watakaopanda ulingoni Julai 22, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam katika mapambano ya kimataifa ya Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati. Katika mapambano hayo ya kimataifa, yaliyoandaliwa na kampuni ya kupromoti mchezo wa ngumi za kulipwa nchini, Solid Rock Tanzania ambayo yatasimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO) chini ya Rais wake, Yassin Abdallah ‘Ustaadh’.

 

Chichi Mawe akiweka pozi.

Chichi Mawe anayetumia mguu wa kulia ‘southpaw,’ masumbwi hayo yatakayorushwa mushabara na Kituo cha Global TV Online kupitia website yake ya www. globaltvtz.com, atacheza na bondia wa Malawi, Israel Kamwamba, Idd Pialali dhidi ya Regin

Champion wa DR Congo na Nasib Ramadhani ‘Pac Man’ akicheza na Mzimbabwe, Tishane Mwadziwana. Risasi Mchanganyiko limefanya mahojiano na bondia huyo ambaye ameeleza maandalizi yake kuelekea kwenye pambano hilo ambalo Watanzania watalishuhudia kupitia katika simu zao za mikononi kwa kuingia kwenye Mtandao wa You Tube kisha kuandika Global TV halafu ku-subcribe ili kuweza kuona matukio mengine yatakayokuwa yakiendelea. “Kiukweli nimejiandaa vizuri kwa sababu tayari nimeshaanza kambi ya maandalizi kwa ajili ya pambano hilo ambalo nataka kuwaonyesha wapenzi wa ngumi kitu kipya.

“Siwezi kukisema sasa hivi hicho kitu zaidi kitaonekana nikiwa ndani ya ulingo, hivyo mashabiki wote wajiandae kushuhudia kutoka katika simu zao maana pambano litarushwa Live na Global TV Online.

 

“Unajua muda mrefu sana sijacheza mapambano makubwa ndani ya Tanzania, sasa kwa kuwa huyu jamaa kajileta mwenyewe, itakuwa moto tena niwashukuru Global Publishers kupitia Global TV kwa kuweza kunirudisha ulingoni.

Unaonekana unamdharau mpinzani wako ? “Hapana sijaonyesha dharau kwake isipokuwa nasema kile ambacho
kipo kwa sababu mimi ni bondia wa muda mrefu mwenye rekodi ya kuwapiga familia ya Matumla yaani baba na mtoto. “Sasa kwa nini niogope kwa mtu mgeni ambaye nimeshaangalia anavyocheza na vipi naweza kumpiga ili niweze kutwaa ubingwa ambao utakuwa heshima kwa nchi yangu.

“Mpinzani wangu ni bondia mzuri kwa sababu rekodi zinaonyesha hivyo, naamini atanipa changamoto kubwa ya kuweza kurudisha makali yangu, ila lazima akae. Nini siri ya kuipiga familia ya Matumla?

“Kwanza Mbwana Matumla ambaye ndiye baba, alinipiga mara moja lakini mapambano yaliyobaki ambayo nilicheza naye yote nilimpiga, kabla sijamgeukia mtoto wake Mohammed Matumla.

“Naamini hakuna ambaye hajui kuwa Mbwana ni fundi wa ngumi na awali alinipiga, nilikuwa sijui mbinu zake ila baada ya kutambua nikamchapa katika pambabo la pili na mengine ambayo nilicheza naye.

“Hata Mohammed pia ni bondia mzuri, ambaye mara zote nimemchapa kama baba yake mdogo, maana siku zote bondia bora ni yule anayecheza na bondia bora mwenzake sasa ubora wangu naamini wamechangia.

Mzimbabwe, Tishane Mwadziwana.

 

“Unajua hata katika hili pambano ambalo nitacheza, huyo Mmalawi ni kwa sababu ya kuwa ubora wangu unajulikana hivyo lazima Watanzania wajue kuwa uhakika wa kubakisha ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati upo.

“Lakini huyu mpinzani wangu ana nyota tatu katika viwango vyetu vya mabondia, sawa na mimi sasa ili niweze kuongeza yangu, lazima nimpige niweze kuchukua yake ije kwangu, hilo ndiyo lengo langu kubwa.” Kitu gani ambacho hutoweza kukisahau katika mchezo wa ngumi?

 

“Binafsi sitaweza kusahau pambano langu na yule Mthailand, Sukpraserd Ponpitak mwaka 2014 ambalo nilipigwa kwa uzembe wa promota kwa sababu yeye ndiye chanzo cha kutokea yaliyotokea. “Unajua nilikutana na ngumi kali ya uso ambayo ilinipelekea chini moja kwa moja huku nikiona maluweluwe, ndani ya ulingo kwani nilikuwa sijui kinachoendelea na wengine walisema sitaweza kucheza tena. “Ile ngumi naikumbuka kwa sababu ya promota, hasa kutokana na muda ambao nilisaini mkataba wa pambano lake ilikuwa tofauti ilivyotokea, nilikuwa sijui nalipwa kiasi gani ndiyo niliamua kudai pale ikatokea vile.

 

“Lakini nashukuru niliweza ku-recover salama na kuendelea na mchezo, ila tu kwa kuwa nilikuwa najitunza wakati wote hadi sasa, naheshimu mchezo huu na jambo zuri ni kwamba kampuni nyingi zinahitajika ili kuweza kurudisha huu mchezo kwenye hadhi yake, siyo Global peke yao,” anasema Chichi Mawe. Katika hatua nyingine pambano hilo ambalo halitakuwa na kiingilio kwa mashabiki kutokana na kurushwa mubashara na Kituo cha Global TV, huku wadau na mashabiki watakaopata nafasi ya kuingia ukumbini watakuwa na kadi za mwaliko maalum kushuhudia ‘ndoga’ hizo.

 

Mashabiki na wadau wengine ambao wataweza kuona mubashara mapambano hayo wanatakiwa kuingia katika website ya www. globaltvtz.com ili kuweza kushuhudia live au pia kuingia moja kwa moja katika Mtandao wa You Tube kisha kuandika Global TV Online na ku-subscribe halafu watakutana na alama ya kengele, ambayo wataibonyeza na moja kwa moja kuweza kupata matukio yote yanayorushwa na kituo hicho papo hapo.

 

KAMA UJA SUBSCRIBE FANYA KUBONYEZA HAPA => GLOBAL TV ONLINE

Leave A Reply