Nisamehe Latifa-45

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA

Latifa akaanza kusimulia historia ya maisha yake tangu alipofukuzwa mama yake ambayo alisimuliwa na mzee Issa, alisimulia kila kitu, baada ya kutimuliwa kisa kikiwa ni mimba ya mtu mweusi, akakimbilia kwa mwanaume aliyempa ujauzito ule ambaye naye aliamua kumtimua nyumbani kwake.

SONGA NAYO…

Ilikuwa simulizi yenye kuhuzunisha, wakati mwingine alipokuwa akisimulia, alitabasamu, kuna kipindi alibubujikwa na machozi. Hakutaka kuacha kitu, alimzungumzia Ibrahim, jinsi alivyoutesa moyo wake, alivyomuacha mbele ya msichana mmoja wa Kiarabu, aliumia, alikosa raha, akakata tamaa ya kupenda hivyo kurudi nchini Marekani.

Alipofika huko, akasimulia kuhusu Liban, kila alipokuwa akiwazungumzia watu hao wawili, machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake, aliumia mno, aliteseka moyoni mwake mpaka kipindi kingine alitamani kufa, afe ili asiweze kuteseka tena.

“Pole sana Latifa,” alisema mtangazaji aliyekuwa akimhoji.

“Asante sana, ila ni maisha, Mungu anaporuhusu jambo fulani litokee, huwa anakupa na mlango wa kutokea,” alisema msichana huyo.

Kipindi hicho kilichukua saa moja, alipomaliza, akasimama na kumfuata mzee Issa, akamkumbatia huku akibubujikwa na machozi mashavuni mwake, alipotoka mikononi mwake, akamfuata bi Semeni na kumkumbatia pia.

“Samahani Latifa,” alisema msichana mmoja, alikuwa mfanyakazi wa hapo.

“Bila samahani.”

“Kuna mtu anakuulizia hapo getini.”

“Nani?”

“Anaitwa Ibrahim, amesema kwamba unamfahamu,” alijibu msichana yule.

Latifa alipolisikia jina hilo, moyo wake ukapiga paaa, akakunja uso wa hasira, machozi yakaanza kumbubujika tena, kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kama mkanda wa filamu.

****

Siku Kituo cha Televisheni cha Global kilipotangaza kwamba siku ya Ijumaa wangekuwa na kipindi maalum cha Latifa, Ibrahim alisikia hilo, akawa na hamu ya kutaka kusikia mengi kuhusu Latifa.

Alichokifanya siku hiyo ambayo ndiyo ingekuwa na kipindi hicho ni kumfuata mzee Deo kwa lengo la kumpeleka nyumbani kwake ili aweze kuangalia kipindi hicho, amuoneshe msichana huyo ambaye aliuumiza moyo wake. Alipokutana na mzee huyo, akamchukua na kumpeleka nyumbani kwake.

“Umemleta kufanya nini humu?” aliuliza Nusrat huku akionekana kuwa na hasira, mbaya zaidi akaziba hata pua yake kumaanisha kwamba alikuwa akisikia harufu mbaya.

“Nimemleta, nataka kumuonyeshea yule msichana aliyenipenda, nikaamua kumuacha kwa ajili yako shetani,” alisema Ibrahim kwa kiburi.

“Ndani ya nyumba yangu?”

“Wewe mjinga nini, hebu tupishe na ole wako ulete za kuleta, ndugu zako watakuta maiti tu humu ndani,” alisema Ibrahim, hata Nusrat alipomwangalia mumewe, alijua kwamba siku hiyo alikuwa tofauti, kama ni ng’ombe basi aliota mapembe.

Ibrahim akamchukua mzee Deo na kwenda kutulia naye kochini, akachukua rimoti ya televisheni kisha kuiwasha. Mzee Deo alikaa kitini, hakujisikia kuangalia, hakuwa na amani kabisa kwani jinsi alivyokuwa akimwangalia Nusrat ambaye alikaa pembeni kabisa, alionekana kuwa na hasira mno.

Latifa alivyooneshwa kwenye televisheni, Ibrahim akajikuta akianza kububujikwa na machozi, moyo wake uliumia, kila alipokuwa akimwangalia msichana yule, akagundua kwamba aliitupa almasi jangwani na kuokota bati.

Msichana huyo mrembo, mwenye muonekano wa fedha akaanza kusimulia historia ya maisha yake. Kila mmoja akabaki kimya akimsikiliza, alianza kusimulia kuanzia mbali, tangu mama yake alipofukuzwa nyumbani kwao, alipokwenda nyumbani kwa mpenzi wake, Deo kisha kumfukuza, alionekana kuumia mno.

Je, nini kiliendelea? Fuatilia wiki ijayo.

Loading...

Toa comment