The House of Favourite Newspapers

NISHA, SISTER FAY; KIKI ZA KISHAMBA HAZIKIKI

KWENU mastaa wawili, Salma Jabu ‘Nisha’ na Faiza Omary ‘Sister Fay’, habari zenu? Mkitaka kujua hali yangu, mimi sijambo. Hofu na mashaka ni kwenu nyinyi ambao kitambo kidogo sijawaona laivu kutokana na majukumu yangu na yenu.

Ndugu zangu, nimelazimika kuwaandikia leo barua maana nimeona kiki zenu zilizotikisa wiki iliyopita. Nisha wewe ulionekana umeopoa Mzungu, ukajinadi kuwa ndiyo mwanaume mwenye mapenzi ya kweli, na kwamba huenda ndiye atakayekuoa.

Ukawapaka matope wanaume wa Kibongo kwamba hawana mapenzi ya dhati hivyo angalau sasa umepata tulizo la moyo wako. Ukatambatamba kwamba sasa hautaumiza kama ulivyoumizwa na wanaume kadhaa wa Kibongo ambao wamecheza na moyo wako.

Ghafla, mke wa Mzungu akaibuka na kueleza kuwa hakuna cha uchumba wala urafiki bali alikusaidia ili mtoe video yenu, sijui mpaka sasa unajisikiaje, maana uso una haya. Ninachotaka kukuambia, angalia kiki za kishamba kama hizo hazikiki; ukiendelea kuzifanya utajikuta unashuka badala ya kupanda.

Kuna kiki za ugomvi wa kimapenzi, kiki za mabishano na mtu ambazo kimsingi hata kazi ikitoka, hakuna mtu anayejua nini kimefanyika lakini kwa kiki ile, ndani ya muda mfupi watu wanakushusha na kukuona huna maana; sisiti kukuambia hiyo ni aibu yako.

Huwezi kujinadi ghafla tu kwamba huyo ndiyo mwanaume wako halafu baada ya muda mfupi tu inabainika kwamba si wako, inakuharibia sana.  Hebu fikiria hao wanaume wa Kibongo uliowadisi kuwa hawana mapenzi ya dhati wanakuonaje hivi sasa?Tokeo la picha la SISTER FEY

Nikushauri; fanya kazi nzuri, maana kazi yoyote nzuri iwe ya sanaa au kitu kingine haihitaji kiki za ovyo kama yako. Waswahili husema chema chajiuza kibaya chajitembeza.  Nikirudi kwako Sister Fay, ulionekana na kibenteni, ukajinadi eti ndiyo mpenzi wako wa sasa.

Video zenu za ajabuajabu zikavuja eti mkibusiana, mkiwa kwenye faragha ambapo kimsingi haipaswi watu wazima kama ninyi kufanya uchafu huo hadharani.

Lakini nyinyi mkajitoa ufahamu, mkarusha hadi mazungumzo yenu ya kimahaba ambayo kimsingi pia yamekudhalilisha tu.  Sister Fay wewe umri wako ni mkubwa, haufanani kabisa na yule bwana mdogo. Vitendo vile unavyooneshana naye kimahaba, ni kujidhalilisha.

Hata kama ni kiki, haikujengi. Ona sasa kabla hata watu hawajazua gumzo la kukubali, wanakuponda tu mwanzo mwisho.  Haujaibua mjadala kuhusiana na suala la wewe kuwa na kibenteni zaidi ya baadhi ya watu kukuona huna maana. Jitahidi sana kuangalia kiki zako ziwe ni za kuibu mjadala.

Kesho na keshokutwa hako kabenteni huwezi kuendelea nako, utakapiga chini au katakutumia halafu kakumwage na kukuachia skendo ya video chafu. Sister Fay; nakushauri ujikite kwenye kufanya kazi. Toa nyimbo nzuri na watu wakujue zaidi kupitia kazi na si kiki.

Fanya kazi sana na Watanzania wakikuelewa, hautatumia nguvu nyingi kujinadi lakini ukiendeza kiki halafu kazi zako zikawa ovyo utajiona umerogwa kumbe mwenye kosa ni wewe.  Niwatakie kila la kheri katika kazi zenu na ninategemea kuona mnabadilika, mnafanya kazi zaidi kuliko kutafuta kiki za kishamba.

Erick Evarist.

Comments are closed.