Na Wilbert Molandi | CHAMPIONI |GPL
UONGOZI wa Yanga umefanikisha mipango yao ya kumbakiza kiungo mchezeshaji wa timu hiyo, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima baada ya kufanya naye mazungumzo na kukubali kubaki kuendelea kuichezea timu hiyo.
Mnyarwanda huyo, ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara akiwemo Thabani Kamusoko, Vincent Bossou, Donald Ngoma, Haji Mwinyi na Deogratius Munishi ‘Dida’.
Awali, kulikuwa na taarifa za kiungo huyo kuomba aondoke mwenyewe na kwenda Cyprus ambako alipata ofa kwenye moja ya klabu nchini humo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi, alisema kiungo huyo amebadili maamuzi hataondoka tena na badala yake ataendelea kubaki Jangwani.
“Hadi hivi sasa tayari uongozi umeanza kufanya mazungumzo na wachezaji kadhaa ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu na kati yao, yumo Niyonzima na amekubali kubaki Jangwani msimu ujao wa ligi kuu,” alisema Mkemi.
Alipotafutwa Niyonzima kuzungumzia hilo, alisema: “Hizo taarifa ulizozipata ni za kweli kabisa, nimebadili maamuzi yangu ya kuondoka Yanga na badala yake nitabaki kuichezea kwenye msimu ujao wa ligi.”