Kartra

Niyonzima Aomba Kuondoka Yanga

TAARIFA zinaeleza kwamba, Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima raia wa Rwanda, hajasafiri na kikosi hicho kuelekea Lindi kucheza na Namungo, huku sababu za kutokea hivyo ikiwekwa wazi.

 

Niyonzima msimu huu ameonekana nafasi yake ndani ya kikosi hicho kuwa finyu licha ya Yanga kubadilishwa makocha wanne.

Makocha hao ambao ni Zlatko Krmpotic, Cedric Kaze, Juma Mwambusi na Nasreddine Nabi, wote wameshindwa kumpa nafasi kubwa ya kucheza msimu huu.

 

Jumamosi hii, Yanga ikiwa inatarajiwa kucheza dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi, jana Jumatano iliondoka Dar na kutua Mtwara, kisha wanasubiri kuelekea Lindi tayari kwa mchezo huo.

 

Mtu wa karibu na kiungo huyo, ameliambia Spoti Xtra kwamba: “Tangu Jumamosi Niyonzima ameondoka kambini na hayupo hadi sasa.

 

“Wakati ameona katika kikosi ambacho kilitarajiwa kucheza na Simba hayupo, akaomba ruhusu, wakampa, akaondoka na hajarudi bado ndiyo maana hajaenda na wenzake kucheza na Namungo.

 

Mwenyewe ameweka msisitizo kwamba hawezi kurudi mpaka wamuhakikishie nafasi ya kucheza kwani anaona anapoteza muda tu huku nafasi yake ikiwa finyu. Ameamua bora apumzike kabisa.

 

Alipotafutwa Niyonzima kuthibitisha hilo, aliliambia Spoti Xtra kwamba: “Ni kweli sijasafiri na timu kwenda Lindi kwa sababu niliomba ruhusa kwa kocha nina matatizo ya kifamilia.”

 

STORI: MUSA MATEJA, SPOTI XTRA


Toa comment