The House of Favourite Newspapers

Niyonzima: Haikuwa Rahisi Kuondoka Yanga

0
Kiungo Haruna Niyonzima.

HAIKUWA kazi rahisi kwa kiungo Haruna Niyonzima kuondoka Yanga na ku­jiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akiwa ameichezea timu hiyo kwa takribani miaka sita.

Niyonzima raia wa Rwanda aliichezea Yanga kuanzia mwaka 2011 akitokea Klabu ya APR ya nchini kwao na hadi anajiunga na timu hiyo ya Jangwani, alikuwa miongoni mwa nyota tegemezi kikosini.

Huyu hakuwa tegemezi kwa klabu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Rwanda, bali hata timu yake ya taifa maarufu kama Amavubi ambayo anaichezea hadi leo.

Akiwa katika mahojiano ya Kipindi cha Spoti Hausi kinachorushwa na Global TV Online kila Alhamisi, Niyonzima anayemudu kucheza nafasi nyingi za kiungo, anasema haikuwa rahisi kwake kuondoka Yanga.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo;

SWALI: NINI KILIKUTOA YANGA? MAANA ULIONEKANA UNA MAPENZI NA TIMU HIYO!

NIYONZIMA: Yanga walinifuata na kufanya nao mazungumzo ya awali lakini hatukufikia muafaka mzuri katika maslahi, mimi nilihitaji kiasi fulani cha fedha ili nisaini mkataba mpya, lakini wao hawakuwa nacho na nikawapa muda kama unavyojua ilikuwa ni timu yangu, kwa hiyo nikawapa muda kwa ajili ya kutafuta na kunipatia, muda ukazidi kwenda na mimi nina familia nikashawishika kusaini Simba.

SWALI: ULIJISIKIAJE SIKU ULIPOKALIMISHA USAJILI SIMBA?

NIYONZIMA: Kwanza, lazima niseme wazi kwamba usajili wangu kutoka Yanga kwenda Simba uliniweka katika presha ambayo sikuwahi kuipata katika maisha yangu ya soka. Haikuwa kazi rahisi mimi kuondoka Yanga kwani nilikuwa naondoka mahali nilipopazoea, watu wake nimezoeana nao na kila kitu cha Yanga kilikuwa sehemu ya maisha yangu. Lakini sikuwa na jinsi, nikaondoka.

SWALI: KUNA MALALAMIKO KUHUSU KIWANGO CHAKO CHA SASA SIMBA, HII UNAIONAJE?

NIYONZIMA: Yapo mengi tu, lakini mimi uzuri nimelizoea soka la Tanzania tangu nikiwa Yanga, hivyo najaribu kukabiliana na hayo malalamiko na ninajua mashabiki wa Simba wanatamani kuniona nikicheza nikiwa katika kiwango cha juu kama kile nilichokuwa nakionyesha nikiwa Yanga.

Lakini tatizo linakuja kuwa, nilikosa muda mzuri wa kufanya mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu kama unakumbuka wakati timu inakwenda kambini Afrika Kusini mimi nilikuwa nyumbani Kigali, katika mapumziko, lakini niwaambie Wanasimba wawe wavumilivu watafurahi.

SWALI: KWA MWENDO WA SASA, UNADHANI SIMBA ITATWAA UBINGWA MSIMU HUU?

NIYONZIMA: Upo uwezekano mkubwa wa Simba kuchukua ubingwa, niwaondoe hofu mashabiki wetu kuwa hizi sare mbili tulizopata zisiwape presha ligi bado mbichi tumecheza mechi tano tu, hivyo niwaambie ubingwa unakuja Simba kwani mipango tuliyoiweka ni kuwa tunataka pointi tatu kila mchezo tutakaoucheza.

SWALI: TANGU UMEJIUNGA NA SIMBA, HAUKUWA UMEPOST PICHA UKIWA NA JEZI ZA SIMBA KIASI CHA MASHABIKI KUKULALAMIKIA, HII IMEKAAJE?

NIYONZIMA: Nikwambie tu, mimi sijakuja Simba kupost picha zangu, nimekuja kufanya kazi pekee, hayo mengine ni mambo binafsi lakini hivi karibuni nilipost picha moja na video nikiwa nimevalia jezi za Simba nikiwa mazoezini.

SWALI: HIVI BADO UNA JEZI YA YANGA NYUMBANI?

NIYONZIMA: Yeha! Bado ninayo nyumbani na nimeihifadhi sehemu nzuri tu kwani ni kumbukumbu kwa watoto zangu hapo baadaye kuwa niliwahi kuichezea Yanga licha ya kuwepo na mitandao kama sehemu ya kumbukumbu zao, ujue soka siyo uadui mimi nikiwa Yanga niliwahi kuwa na jezi ya Simba niliyopewa na marehemu Mafisango (Patrick) ambayo alinipa kama zawadi yangu na alikuwa akiivaa sana mke wangu.

SWALI: BADO UNA MARAFIKI YANGA?

NIYONZIMA: Kama nilivyosema mwanzo wengi wanajua soka ni uadui, mimi ninajua ni urafiki, niseme kuwa wengi siwasiliani nao kama ilivyokuwa mwanzoni, lakini nakumbuka wakati nikiwa Yanga mimi nilikuwa na marafiki wengi wa Simba tena tulikuwa tunakutana na kukaa na hao walikuwa wakikubali uwezo wangu wa ndani ya uwanja.

SWALI: ILIKUWAJE KAZIMOTO AKAKUVULIA JEZI NAMBA NANE NA KUKUPA WEWE?

NIYONZIMA: Ni heshima kubwa aliyonionyeshea Kazimoto, kwanza naheshimiana naye sana na kingine naheshimu uwezo wake mkubwa alionao, halafu niseme kitu kingine mimi nilianza kujuana naye tukiwa tunakutana kwenye michuano ya majeshi na siyo Simba, hivyo nimepanga kumfanyia kitu kimoja kikubwa sana ambacho ni ‘sapraizi’ kwake na nitakachomfanyia hataweza kukisahau maishani mwake.

Stori: Wilbert Molandi,Championi Jumamosi

Leave A Reply