Niyonzima: Nitaipa Yanga Ubingwa

KIUNGO mtoa burudani awapo uwanjani, Haruna Niyonzima, amesema yupo katika kikosi cha Yanga ili kuipa ubingwa timu hiyo na si kitu kingine.

 

Kauli ya Niyonzima imekuja siku chache baada ya kuenea kwa taarifa za yeye kugoma kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo Yanga ilifungwa na Mtibwa Sugar kwa penalti 4-2, Alhamisi iliyopita na kuondolewa mashindanoni hatua ya nusu fainali.

 

Niyonzima amejiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo akitokea AS Kigali ya Rwanda. Hii ni mara ya pili kwa kiungo huyo kuitumikia Yanga, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2011 akitokea APR ya Rwanda, mwaka 2017 akaachana na Yanga na kutua Simba ambapo alicheza misimu miwili, akarudi kwao Rwanda kuichezea AS Kigali.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Niyonzima alisema: “Watu wanajisemea mambo mengi kuhusu
mimi, lakini ukweli nadhani hawaufahamu, ukisema naigomea Yanga litakuwa ni suala la ajabu sana kwangu.

 

“Baada ya kufi ka hapa nilifanya mazoezi siku mbili tu na Yanga kisha nikacheza mechi dhidi ya Simba, hivyo isingekuwa rahisi tena kwenda kwenye michuano bila kufanya maandalizi.

 

“Watu wanatakiwa watambue kwamba siwezi kugomea kazi yangu, maana nipo Yanga kuhakikisha inachukua ubingwa wa ligi na si kitu kingine na ndiyo maana nilibaki kujifua zaidi,” alisema Niyonzima


Loading...

Toa comment