Nje unapendeza, ndani unachekesha, utaimbwa mkoleni

loversHaya hayaaa! Nimetua tena kama dege la kivita, najua kiroho pa! jamani mi si Izrael mtoa roho, bali shoga yako namba moja anayeijali ndoa yako. Angelijua hilo, basi angeniganda kama ruba. Mapenzi yangu kwenu ndiyo yanayonifanya niwape makavu nisiyochanganya na maji,  japokuwa yanawauma, lakini mkiyafanyia kazi mtacheka mwisho na kusahau ni mimi mliyenichukia.

Leo shoga nataka nikuume sikio, inawezekana hujui lakini shoga unaibomoa nyumba yako kwa mikono yako mwenyewe. Wahenga walisema mjenga na mvunjaji wa nyumba ni wewe mwenyewe. Shoga umeolewa au una mpenzi unayekaa naye?

Inawezekana katika maisha yako kuna vitu ulikuwa ukivitamani muda mrefu na baada ya kuvutwa karibu,  basi unaona huo ndiyo muda mzuri wa kutimiza uliyoyakosa.

Haya nayosema si ya kubuni, yanaweza kukugusa hata wewe, utakuta mwanamke ukimwangalia amechafuka shingoni mikufu ya dhahabu, mikononi bangili, vidoleni pete,  masikioni nako kumechafuka kila sikio moja lina tundu zaidi ya matano na kila tundu lina hereni ya dhahabu.

Nakubaliana nanyi mwanamke kujiremba, hebu ingia ndani mwake chumbani kuna kitanda tu hata shuka matatizo. Nyumba yake haijali zaidi ya kujijali yeye ili aonekane mbele ya macho ya watu. Mumewe uwezo wake mdogo lakini kwa vile anajijali mwenyewe hana akili ya kumshauri mambo ya kimaendeleo wakipendezeshe chumba chao.

Lakini unachojua wewe kila kizuri uwe nacho, ukawakonge kwenye sherehe, sherehe zote hukosi umemtia madeni mumeo kila kona anadaiwa. Kweli mtaani unatingisha kwa kulipuka na migold na mibazee. Lakini huwezi kuongozana na mumeo au mwanao kwa kuona aibu kwani wao wapo kama wakimbizi lakini wewe unameremeta.

Umekuwa unamnyima raha mwenzio, kila anachokipata unaona ni haki yako kupewa wewe kununua micheni, mipete na hereni za dhahabu ila kuwakonga wenzako. Humjali mumeo viatu vyake vimelala yombo kama vimepigwa jeki ana shati moja, suruali kama ngozi, mwanao naye anatembea makalio nje, nguo nzuri anavaa mkienda safari nayo ilinunuliwa siku ya sikukuu.

Shoga hakuna maisha ya hivyo, kusifika kwenye macho ya watu wakati kwako kunateketea ni ujinga. Humkaribishi mtu ndani kwa kuogopa aibu ya ndani kwa vile unawapeleka tumbo joto mtaani.

Kuna siku roho iliniuma baada ya mwanamke mmoja aliyekuwa amekaa nje ya nyumba yake na shoga yake, mara alirudi mumewe akitoka kazini.

Hakumpokea hata alipowasalimia alimwitikia kwa kujilazimisha, yule bwana aliingia ndani na kumuacha mkewe akiendeleza stori si ndiyo akaitwa ndani. Alinyanyuka kama analazimishwa baada ya muda alirudi na kumfanya shoga yake amuulize kwani wito ule ulikuwa na dalili zote za kuitwa na mumewe.

“Shoga ndo mumeo nini?”

“Atawahi! Shemeji yangu, mdogo wake na mume wangu, ametoka kijijini basi anajisikia raha kuniita mke wake.”

“Mmh! Nilitaka kushangaa Mwaju ninayekufahamu kuwa na mwanaume kama mfagizi wa barabara.”

Jamani nakuoneni mnacheka, usicheke inatisha kwa mtu kumkana mumewe kwa vile tu hayupo smati na haendani na yeye. Watu wakikuangalia wewe na mumeo kama mbingu na ardhi. Kila nguo nzuri inayotoka unayo, sare yoyote ya shughuli za mashoga zako unazo. Mumeo hana haki ya fedha yake akipokea unapanga wewe na kujipendelea wewe kwa vile mumeo ushamwinamisha kwa waganga basi unafanya unavyotaka.

Shoga nataka kukueleza huko ulipomwendea kwa waganga ili kumgeuza punda, ipo  siku atabumburuka na dunia utaiona chungu. Nataka kuwaeleza kitu kimoja mashoga zangu, kupendeza ni haki ya kila mmoja basi kinachopatikana kidogo nunua unachotaka kingine mpendezeshe mumeo na mwanao bila kukisahau chumba chako ili unapomkaribisha shoga yako ndani achanganyikiwe na kukuongezea heshima mtaani. Lakini nje unapendeza ndani unachekesha utaimbwa mkoleni.

Ni mimi anti Nasra Shangingi Mstaafu.


Loading...

Toa comment