The House of Favourite Newspapers

Njemba Anusurika Kuuawa kwa tuhuma za Mauaji

0

JAMAA mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, amejikuta matatani baada ya kusukumiwa madai ya mauaji.

 

Tukio hilo ambalo lilipigwa chabo na paparazi wetu live, lilitokea maeneo ya stendi ya Mjini Ijumaa iliyopita.

 

Awali, paparazi wetu alishuhudia mama mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Amina akiwa amesimama kwenye kituo hicho akionesha dalili za kuwa miongoni mwa wasafiri waliokuwa akisubiri mabasi.

Ghafla, Njemba aliyekutwa na mkasa wa kunusurika kuuawa na raia wenye hasira kali kwa madai ya kuwa ni muuaji, alipita mahali alipokuwa amesimama yule mama.

 

Kupita kwake kulikozaa hali ya kutazamana uso kwa uso; ikatokea kama sumaku zimekutana ambapo kila mmoja alionesha kushangazwa na mwenzake kuwepo eneo hilo.

Ghafla jamaa akaona ‘isiwe tabu’ akaanza kutimua mbio na kuleta sintofahamu miongoni mwa watu akiwepo mwandishi wetu.

 

Kabla njemba huyo hajapiga hatua nyingi na kutokomea, mama huyo aliibuka na sauti ya kuomba msaada “Huyoo, huyooo huyoooo, muuaji.”

Kelele hizo zilizidi kuvuta hisia za watu waliokuwepo karibu naye ambapo wengine walimuuliza kwa haraka: “Kafanya nini?”

 

“Huyo kaka amefanya mauaji Mikumi na anatafutwa, kumbe kakimbilia huku Morogoro mjini,” alisema mama huyo wakati huo pilikapilika za watu kumfukuza njemba huyo zikiwa zimeshaanzishwa na wale wanaojiita ‘wananchi wenye hasira kali’.

Kama unavyojua ‘mwano’ unavyokusanya watu kama nyuki kutoka kila kona, ghafla jamaa alijikuta akiwa amezingirwa na watu na kuanza kupata kipigo kikali.

Akizungumza na mwandishi wetu, mmoja wa watu walioshiriki kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo alisema, aliposikia kelele hakutaka kusubiri, bali ni kumfukuza huyo mwanaume huku akidhani kuwa ni mwizi.

“Mimi sikutaka kusubiri, nilipoona anakimbia, nikamuunganishia na kufanikiwa kumkamata. Nilijua kamuibia bi mkubwa.”

 

Hata hivyo, baada ya kundi la watu kufanikiwa kumkamata njemba huyo aliletwa kwa mama huyo huku wengi wakiwa na imani kuwa ni mwizi lakini majibu waliyopewa, yaliwashangaza.

“Amekuibia nini mama?” Kijana mmoja aliuliza.

“Hajaiba, huyu baba ni muuaji, kamuua ndugu yangu eneo la Mikumi akatoroka. Nashangaa kumkuta hapa Morogoro.”

 

Aidha, wakati wengine wakitaka kujua sababu za nini kilitokea hadi jamaa kutiwa matatani, baadhi walikuwa wakiendelea kumpiga kwa kutumia ngumi, mateke na vipande vya mawe.

Pamoja na kuzongwa na watu wengi, bahati ilikuwa kwa njemba huyo ambapo kundi la watu wengine liligeuka na kuanza kumtetea na kutaka asipigwe na kwamba apelekwe polisi kutokana na tuhuma zake kuwa nzito.

 

Wakati mzozo ukiendelea na kipigo cha mbalimbali kikimpata jamaa huyo, askari wa usalama barabarani waliokuwa karibu na eneo la tukio, walikuja kuongeza nguvu na kufanikiwa kutuliza hali ya hewa.

Busara ilikuwa ni kwamba, mtuhumiwa pamoja na huyo mama, wapelekwe Kituo cha Polisi cha Kati kwa ajili ya mahojiano zaidi.

 

Mwanahabari wetu alijaribu kuzungumza na mama huyo ili kujua zaidi tukio analodai kufanywa na mtuhumiwa huyo, lakini haikuwezekana kutokana na mama huyo kuangua kilio na kuahidi kwenda kuzungumza kituoni.

Ingawa mwandishi wetu aliongozana na mtuhumiwa pamoja na yule mama hadi kituoni, lakini hakufanikiwa kupata maelezo yao kutoka polisi.

 

Kwa kuzingatia utaratibu wa kipolisi, mwandishi wetu alifika ofisini kwa Kamanda wa Polisi Morogoro, Wilbroad Mutafungwa ili kupatiwa maelezo ya kile kilichotokea, lakini kamanda huyo hakuwepo na kwamba msaidizi wake alisema mkuu wake alikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, hivyo isingekuwa rahisi kuzungumzia jambo hilo.

 

STORI| Dunstan Shekidele, Risasi

Leave A Reply