NJEMBA YAMKUTA MAZITO MAKABURINI

 

USIOMBE kutaitiwa na wananchi wanaoitwa wenye hasira kali! Njemba mmoja aliyejulikana kwa jina la Kingdoom mkazi wa Msamvu mkoani Morogoro, yamemfika mazito akiwa kwenye eneo la makaburi ya Kolla. 

 

Shuhuda wa tukio alidai kuwa, Kingdoom alifika eneo la tukio kwa lengo la kuiba misalaba kwenye baadhi ya makaburi hayo ili akaiuze kama chuma chakavu na kujipatia fedha. Akiwa katika eneo hilo la makaburi alfajiri na mapema, njemba huyo alianza kazi ya kung’oa msalaba mmoja baada ya mwingine na kuikusanya eneo moja tayari kwa kutokomea nayo.

 

Mara paaap; msemo wa ‘za mwizi arobaini’ ukatimia kwake: “Unafanya nini hapa?” Kingdoom aliulizwa na alipoinua kichwa amtazame aliyemuuliza, aliona ‘watu kama wote’ wakiwa wamemzingira.

Bila kuchelewa watu hao wenye hasira kali waliokuwa na majembe, sululu, chepe na mapanga walianza kumshambulia kwa kipigo huku adhabu za ‘ruka kichura’ nazo zikitolewa. Kama Waswahili wasemavyo ‘penye wengi haliharibiki neno; hoja ya “Tumuue na kumzika ilipotolewa, wengine walipinga na kumpigia simu mwandishi wetu ambaye naye aliwataarifu polisi na wote kuelekea eneo la tukio.

Baada ya mwandishi wetu na polisi kufika eneo la tukio, walimkuta Kingdoom akiwa ‘amechakaa vya kutosha’ na walipouliza watu waliokuwepo hapo kimetokea nini; ndipo mmoja kati ya mashuhuda (Jina halikufahamika) aliwaambia polisi:

“Sisi tulikuja kuchimba kaburi, tulipofika tukamuona huyu jamaa anang’oa misalaba, tukajua ndiyo hawa wanaoiba misalaba ya watu, tukambana.” Kingdoom alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu madai ya wizi, alikiri na kusikitikia kukamatwa siku yake ya kwanza ya kazi.

“Yaani leo ndiyo siku yangu ya kwanza, sijawahi kuiba,” alisema Kingdoom huku akitweta kwa kipigo alichokuwa amepewa. Hadi anatiwa mbaroni, tayari alikuwa ameshajikusanyia misalaba ipatayo 30 ikiwa na majina ya marehemu ambayo alisema alitaka kuiuza kama vyuma chakavu kwa bei ya shilingi 1,000 kwa kila kilo moja.

Wenyeji wa maeneo ya Msamvu ambako pia ilizikwa miili ya marehemu zaidi ya mia waliokufa kwenye ajali ya lori la mafuta, wamekuwa wakilalamikia wizi wa misalaba ambao unasababisha utambulisho wa makaburi ya ndugu zao kupotea.

Aidha, kutokana na tukio hilo la kunaswa na misalaba hiyo ya wizi; Kingdoom pamoja na mmoja wa walinzi wa makaburi hayo yanayomilikiwa na manispaa ya Morogoro walichukuliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.

Stori: Dustan Shekidele Morogoro


Loading...

Toa comment