The House of Favourite Newspapers

NJIA 6 KUZUIA MAUMIVU YA TUMBO KIPINDI CHA HEDHI

KAMA ilivyo kwa wanawake wengi, inapofikia wakati wa hedhi, huwa wanapatwa na maumivu makali sana ya tumbo, likiwa limezoeleka kama tumbo la uzazi na maumivu haya huwasababishia kukosa amani kabisa, kuachana na shughuli zao za kikazi, masomo na mambo mengine mbalimbali lakini kwa bahati nzuri maumivu haya yanaweza kuzuilika. Lakini kabla hatujatibu tatizo, inabidi tuufahamu mzizi wake kwanza.

CHANZO CHA MAUMIVU YA TUMBO

Maumivu ya tumbo la uzazi (Uterus) hutokana na kukaza na kukakamaa kwa misuli ya tumbo hilo ili kuwezesha uondoaji wa kuta za tishu zenye damu zilizojishikiza wakati wa hedhi.

Kitendo hiki huchangiwa na kemikali aina ya homoni zinazoitwa prostaglandins ambazo ndizo zinahusika na maumivu na kujisikia muwako wa moto na ndizo huanzisha kusinyaa kwa misuli ya Uterus. Kiwango cha prostaglandins kinapozidi, ndivyo maumivu yanavyoongezeka zaidi.

Sasa, baada ya kuugundua mzizi wa tatizo, tunaweza kutafuta njia za kuondokana na tatizo. Kwa maana hiyo, tukiweza kudhibiti kiwango cha prostaglandins, au kuifanya misuli ya tumbo ilegee badala ya kusinyaa na kujikaza tutakua tumelidhibiti tatizo. Njia za kufanya kuondokana maumivu ya tumbo wakati wa hedhi.

FANYA MAZOEZI

Unaweza kulichukulia kama mzaha lakini ni jambo la msingi sana kwa afya yako, kufanya mazoezi hata ya kutembea umbali flani, kukimbia au kazi yoyote inayohitaji nguvu, moyo wako husukuma damu nyingi kwa kasi zaidi katika mwili; hii husaidia kutoa kemikali nyingine inayoitwa ‘Endorhins’ ambayo hufanya kazi kinyume na prostaglandins na kuzuia makali yake, hivyo kuzuia maumivu ya tumbo na kuurudisha mwili katika hali ya msawazo wa kawaida.

Jaribu kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki, kama ulikua ukisumbuliwa na maumivu haya, matokeo utayaona.

TIA JOTO KULEGEZA MISULI

Joto husaidia kulegeza misuli ya Uterus iliyojikaza ambayo hasa ndio chanzo cha maumivu. Kuna vifaa mbalimbali vya kisasa kwa ajili ya kazi hii, kama vile ThermaCare na Bengay, ambavyo vinatumika zaidi ya mara moja.

Lakini kama huwezi kuvipata hivi, usijali, tumia njia za kawaida kama kuweka maji ya moto ndani ya chupa ya plastiki na kuanza kujikanda nayo sehemu za tumboni zenye maumivu, itakusaidia.

PATA VITAMIN D

Siku zote kinga ni bora kuliko tiba, hivyo, kwa kuhakikisha unakua na vitamin D3 (cholecalciferol) muda wote, itakukinga na maumivu haya.

Utafiti uliofanyika kule Italia, imeonekana kuwa wanawake waliopewa dozi ya kutosha ya vitamin D3, maumivu yao yalipungua kwa asilimia 40. Vitamini hiyo hupatikana kutoka kwenye jua la asubuhi na kula vyakula kama maini ya ng’ombe, kiini cha yai na samaki wenye mafuta.

UNYWAJI WA KAHAWA

Kahawa ina Caffeine ambayo hufanya kazi ya kuminya mirija ya damu na kuongeza shinikizo la damu na kwa kuinywa huweza kuminya pia mirija ya damu katika misuli ya uteras na kuzidisha maumivu mara dufu hivyo, hata kama ni mnywaji mzuri wa kahawa, jaribu kuacha walau ile wiki ya hedhi na matokeo utayaona.

MSHINDO (ORGASM)

Kufikia kilele wakati wa tendo la ndoa husaidia kuondoa maumivu mengi ikiwa ni pamoja na maumivu ya tumbo la uzazi. Wakati wa mshindo msukumo wa damu huongezeka na kutoa kemikali tuliyoijadili mwanzoni iitwayo Endorphins, ambayo husaidia kutuliza kukaza kwa misuli ya uterus na pia kuuweka mwili katika hali ya msawazo na kukupatia usingizi mwanana kabisa.

USHAURI

Unatakiwa kula mboga za kijani kwa wingi ili kuongeza madini ya calcium na magnesium ambayo ni muhimu sana kwa afya ya misuli, vilevile usisahau kuwaelimisha wenzako kuhusu ujumbe huu.

 

Comments are closed.