The House of Favourite Newspapers

NJIA ZA KUEPUKA KISUKARI (DIABETES)

UGONJWA wa kisukari (diabetes) unaongezeka haraka sana na umekuwa janga ulimwenguni pote. Kuna aina kuu mbili za kisukari;  Aina ya kwanza huanza utotoni na hadi sasa madaktari hawajui jinsi ya kuzuia. Makala haya yanazungumzia aina ya pili ambayo imeathiri asilimia 90 ya watu walio na kisukari Ingawa zamani aina ya pili ya kisukari ilihusishwa tu na watu wazima, hivi sasa imewaathiri pia watoto. Lakini mtu anaweza kujikinga ili asipatwe na kisukari.

Kisukari ni nini? Kisukari ni ugonjwa unaotokana na mtu kuwa na sukari nyingi kupita kiasi kwenye damu. Ugonjwa huo huvuruga utaratibu wa kuingiza sukari ndani ya chembechembe za damu kutoka kwenye damu kwa kuwa chembechembe za damu huhitaji sukari ili kupata nishati.

Sukari ikizidi mwilini huharibu viungo muhimu na husababisha hitilafu ya mzunguko wa damu na nyakati nyingine inaweza kufanya mtu akatwe vidole vya miguu au mguu. Pia husababisha upofu na maradhi ya figo.

Wagonjwa wengi wa kisukari hufa kutokana na mshtuko wa moyo (heart attack) au kiharusi. Mafuta mengi kupita kiasi mwilini huchangia sana mtu kupata kisukari. Mafuta yaliyokusanyika tumboni na kiunoni ni ishara ya uwezekano wa kupatwa na kisukari.

Mafuta katika kongosho na ini huvuruga uwezo wa mwili kudhibiti kiasi cha sukari kwenye damu. Ili kuepuka kupatwa na kisukari, fuata hatua tatu zinazoweza kukusaidia usipatwe na kisukari. Mosi; pimwa kiwango cha sukari kwenye damu ikiwa una uwezekano mkubwa wa kupata kisukari.

Mara nyingi aina ya pili ya kisukari huanza baada ya hatua inayoitwa prediabetes yaani, ongezeko la kiwango cha sukari kwenye damu. Hatua hiyo ni hatari ingawa ugonjwa wa kisukari unaweza kudhibitiwa, lakini hauwezi kutibiwa.

Kwa upande mwingine, watu walio na kiwango cha juu cha sukari kwenye damu huenda wasitambue dalili za ongezeko la sukari kwenye damu. Kulingana na ripoti mbalimbali, karibu watu milioni 316 duniani kote wana kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu; ingawa wengi wao hawajui wana kiwango hicho

Hata hapa Tanzania kuna watu wana ugonjwa huu, lakini hawatambui na ndiyo maana tunashauri watu kupimwa kisukari hata kama huna dalili. Ongezeko la sukari kwenye damu ni hatari. Mbali na kuwa kisababishi cha kisukari, hali hiyo imehusishwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa akili uitwao dementia.

Kama wewe ni mnene kupita kiasi, hufanyi mazoezi au una watu katika ukoo wako walio na kisukari, huenda tayari una kiwango cha juu cha sukari kwenye damu, lakini hujui kwa kuwa hujawahi kupima. Nenda kapime sasa. Unaweza kujua kiwango chako cha sukari ukipimwa damu.

KULA VYAKULA VYENYE LISHE

Unaweza kufaidika ukifanya mambo yafuatayo; Punguza kiasi cha chakula unachokula. Badala ya kunywa vinywaji vyenye sukari nyingi au vinywaji vyenye kaboni kama vile soda, kunywa maji, chai au kahawa na ikiwezekana isiyo na sukari.

Kula vyakula vya nafaka ambayo haijakobolewa badala ya vyakula vilivyochujwa sana viwandani. Kula nyama isiyo na mafuta mengi, samaki, njugu, karanga, na maharage. Pia kula matunda kila siku hasa tikitimaji.

USHAURI

Kufanya mazoezi kunaweza kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu na kukusaidia uwe na uzito unaofaa. Fanya mazoezi kila siku.

Huwezi kubadili chembechembe za damu yako za urithi, lakini unaweza kubadili maisha yako. Utafaidika sana ikiwa utajitahidi kutunza afya yako. Kisukari kinadhibitika kwa ushauri piga siku au tuma ujumbe kwa namba hiyo.

Comments are closed.