The House of Favourite Newspapers

Njia zote Dar leo zielekee Uwanja wa Taifa

TANZANIA leo Jumapili jioni itashuka Uwanjani Jijini Dar es Salaam kuandika historia ambayo vijana wengi wa kizazi kipya hawakuwahi kuiona. Inacheza kuwania kufuzu fainali za Afcon ambazo imethibitishwa zitapigwa mwaka huu nchini Misri.

 

Inacheza na Uganda ya straika Emmanuel Okwi ambaye tumezoea kumuona akiwa kwenye jezi ya Simba. Stars ipo kundi L lenye timu zenye historia nzuri kisoka za Uganda, Cape Verde na Lesotho.

 

Mechi hiyo ya Stars ni ngumu kwani Tanzania inahitaji kushinda kwani hata wapinzani wake bado wana nafasi ya kufuzu. Uganda ambao ni majirani zetu ndio ambao wameshafuzu.

 

Stars yenye pointi tano inahitaji kwa vyovyote vile kushinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri bila kusikilizia nini kitatokea upande wa pili. Kama Stars ikishinda mchezo wa leo itafikisha pointi nane ambazo hazitaweza kufikiwa na Cape Verde na Lesotho kama watatoka sare au Lesotho akifungwa.

 

Cha muhimu ambacho Stars wanapaswa kufanya leo Jumapili ni kutuliza akili uwanjani na kufanya kile vitu sahihi na kuhakikisha ushindi unapatikana ili kumaliza kazi na kuwapa raha mashabiki wa Tanzania. Mashabiki kibao watajazana Taifa kutoa sapoti kwavile kila sehemu Watanzania wamekuwa wakihamasishana kuhakikisha Mganda anapotea leo na Stars inafuzu.

 

Ambao hawafika Uwanja watakuwa wakiwaombe Stars kila la kheri na ushindi upatikane tena mnono kwa heshima ya Tanzania. Kama kweli wachezaji wakiweza kutimiza azma hiyo ya mashabiki, tunaamini Tanzania nzima itazizima leo usiku. Ni ndoto ya kila Mtanzania na mwana Afrika Mashariki kuona Tanzania na Uganda zinacheza Afcon mwakani kwani Stars katika miaka ya hivikaribuni ilikwama kabisa na kushindwa kufikia hatua hiyo.

 

Kimahesabu Uganda ameshafuzu kutokana na kuzichanga karata zake mapema kwa kuwatumia wachezaji wake wazoefu wa ndani na nje ya nchi. Tunaamini kwamba kwa Stars hii tuna kila sababu ya kufuzu kutokana na kuwa na wachezaji wenye uelewa na ndoto za kufika mbali wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta.

 

Ni jukumu la kila Mtanzania kuiombea timu yetu kila kheri mwenyezi mungu awape wepesi vijana wetu wafanye kile ambacho kila shabiki anakihitaji. Stars ikifuzu Afcon itakuwa ni mwanga mzuri kwa soka letu na mauzo ya wachezaji wetu kwani ndiyo mashindano makubwa kwenye ukanda wa Afrika ambayo yanatazazwa na mawakala wengi kutokana na ubora na umaarufu wake.

 

Hivyo ni rahisi sana kuyatumia mashindano hayo kuitangaza nchi na wachezaji wenyewe binafsi kwani ni tukio ambalo kwa miaka mingi vijana wa kizazi kipya wamekuwa wakiliona kwenye runinga tu kwa kushangilia timu za mataifa mengine. Shimeshime tumwagike kwa wingi kwenye Uwanja wa Taifa tukasapoti vijana wetu waishangaze Duniani. Tuna kila sababu ya kuishangilia timu yetu, tuna kila sababu ya kushinda. Ni zamu yetu kwenda Afcon.

Comments are closed.