The House of Favourite Newspapers

Njooni Uwanjani Ila…

0

UNAAMBIWA Simba wamepanga kuanza mechi yao ya leo dhidi ya Plateau kwa kasi kubwa kiasi cha kuwafanya wachezaji wa timu pinzani kutakiwa kuandaa leso ‘kitamba cha kujifutia’ kwa ajili ya kujifuta jasho mara kwa
mara.

Simba leo itakuwa Dimba la Mkapa, Dar katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau ya
Nigeria, kumbuka katika mchezo wa kwanza uliopigwa Jos nchini huko Simba walishinda bao 1-0 lililowekwa kimiani na Clatous Chama.

 

Wababe Simba wataingia katika mchezo wa leo mida ya saa 11 jioni wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kutoa sare michezo miwili iliyopita ya michuano hiyo ikiwa nyumbani, ilibanwa na TP Mazembe ya DR Congo ambapo mechi yao iliisha suluhu kisha sare ya 1-1 dhidi ya UD Songo ya Msumbiji.

 

Simba imekuwa ikiwategemea zaidi viungo washambuliaji wenye kasi kama Chama, Luis Miquissone pia anaweza
akaanza na Bernard Morrison ambaye naye amtengenezea nafasi za kufunga nahodha, John Bocco.

 

Sasa kuelekea mchezo huo wa marudiano, uongozi wa Simba umeahidi ushindi mzito ikiwemo kucheza soka la kuvutia mithili ya ‘Tik Taka’ ambalo ni aina ya soka linalopatikana katika timu ya Taifa ya Hispania na Klabu ya
Barcelona.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa licha ya kutambua ugumu wa timu hiyo lakini wamepanga mipango ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi mzito pamoja na kucheza
soka safi na la kuvutia yaani ‘Tik Taka’.

 

“Japo tunatambua kuwa Plateau ni timu nzuri lakini kwa Mwanasimba yeyote unatakiwa kuja ushuhudia
Simba ikishinda kwa ushindi wa kishindo bila kusahau soka la kuvutia mithili ya ‘Tik Taka’, hii ndio staili yetu ya soka burudani kwetu ni nyumbani,” alisema Manara.

 

Naye Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, ambaye alizungumza juu ya maandalizi ya timu hiyo kuelekea mchezo huo wa marudiano, alisema kuwa kikosi kipo tayari kwa ajili ya mapambano na kila kitu kinaenda
sawa chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck.

 

“Kila kitu kipo sawa, timu ina maandalizi ya kutosha, hivyo naweza kusema kuwa tumejiandaa vizuri kwa ajili ya
mechi yetu ya marudiano chini ya usimamizi wa kocha mkuu Sven Vandenbroeck na kilichobaki ni mpambano ambapo malengo yetu ni kuhakikisha tunapata ushindi na kusonga mbele,” alisema kocha huyo.

 

Simba ikifanikiwa kupita hapa itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Costa do Sol ya Msumbiji ikiwa ni hatua ya mtoano na ikipita hapo inaenda hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Stori:Marco Mzumbe

Leave A Reply