BENKI ya NMB imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ikiwa ni udhamini wao katika michezo mitatu, yaani mchezo wa ngumi, mieleka pamoja na mchezo wa riadha.
Udhamini huo wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 18, umekabidhiwa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi, Biashara ndogo na za Kati, Filbert Mponzi kwa viongozi wa JWTZ.
Aidha akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mponzi alisema vifaa hivyo vya michezo vilivyotolewa na NMB ni sehemu ya udhamini wa Benki ya NMB kwa michezo ya ngumi, mieleka pamoja na riadha.
Aliongeza kuwa, Benki ya NMB inaushirikiano mkubwa na wa muda mrefu ambao umekuwa na faida kwa pande zote huku ukiendelea kuimarika siku hadi siku.
“Kwa niaba ya NMB tunaomba mtuwakilishe vema na tutafurahi zaidi mkirudi hapa na medali za dhahabu, tutakuwa na furaha zaidi kwani si tu mmeshinda bali benki yetu itakuwa imeshiriki kufanikisha ushindi huo,” alisema Bw. Mponzi akikabidhi msaada huo.
Alibainisha kuwa NMB imekuwa ikishirikiana na JWTZ kudhamini michezo mbalimbali, jambo ambalo linaendelea kuboresha mahusiano mazuri kati ya pande zote.
Michezo ya Majeshi Duniani, World Military Games inayoshirikisha majeshi mbalimbali ulimwenguni, inatarajia kufanyika nchini China katika Jiji la Wuhan hivi karibuni.
Comments are closed.