Wanawake wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri Tanzania (TUICO), wametakiwa kuvutiwa na mafanikio kitaifa na kimataifa ya Hati Fungani ya Jasiri ya Benki ya NMB ‘NMB Jasiri Bond,’ na kuyatumia kama chachu ya kuendelea kuwa wateja waaminifu wa benki hiyo ili kuwa sehemu ya mnyororo wa wanufaika wa huduma zenye lengo la kusaidia ustawi wao kimaisha na kukua kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Joanitha Mrengo, alipomwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, katika semina ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wanawake ambao ni Wanachama wa TUICO Mkoa wa Morogoro, iliyofanyika kwa siku moja, ikihudhuriwa pia na viongozi wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na kudhaminiwa na benki hiyo.
Aprili mwaka jana, NMB ilihitimisha mauzo ya Hati Fungani ya Jasiri kwa kuvuna kiasi cha Sh. Bil. 74 na kuvuka lengo la kukusanya Shilingi bilioni 25 pesa zilizotumika kutanua wigo wa utoaji huduma za mikopo kwa kampuni zinazoendeshwa na wanawake, ama kampuni zinazozalisha bidhaa zinazowagusa wanawake nchini.
Ni mafanikio yaliyoipa NMB tuzo mbalimbali, zikiwemo za Hati Fungani Bora ya Mwaka iliyotolewa na Waandaaji wa Tuzo za Kimataifa za Mitaji kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati kwa kushirikiana na Jukwaa la Ufadhili wa Ujasiriamali (SME’s Finance Forum), pamoja na Tuzo ya Platinum ya Kundi la Dhamana Endelevu iliyotolewa nchini Cambodia, kote ikitambulika kama hati fungani wezeshi kwa wanawake, kiasi cha kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Luxemburg (LuxSE), ambalo ni moja ya masoko makubwa ya hisa duniani.
Akizungumza wakati akifungua semina hiyo, Mrengo alisema mafanikio hayo, pamoja na kutambuliwa kwa benki yake kuwa miongoni mwa taasisi kinara katika mgawanyo wa kiuchumi kwenye suala la kijinsia (EDGE Certificate), ambako NMB ni taasisi ya kwanza Afrika kutunukiwa cheti, vinapaswa kutazamwa kwa jicho la ziada na wanawake wote nchini, wanaopambania ukuaji wao kiuchumi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa TUICO, Tamim Salehe, aliishukuru NMB kwa kushirikiana na chama chake katika kuwanoa wanawake wanachama wa mkoa wa Morogoro, huku akiwataka washiriki wote kuitumia vema semina hiyo sio tu kwa kuzingatia maelekezo, bali pia kujenga mtandao wa kiushirikiano baina yao ili kusaidiana maarifa ya utatuzi wa changamoto mahali pa kazi ama biashara zao.