The House of Favourite Newspapers

Nmb Yazindua Kampeni ya Umebima 2023, Elimu Zaidi Yatolewa

0
Kutoka Kushoto: Mkuu wa Idara ya Bima  Benki ya NMB, Martine Massawe; Kamishna wa Bima nchini, Dkt. Baghayo Saqware; Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara NMB, Filbert Mponzi wakizundua kampeni ya Umebima jijini Mbeya jana.

Katika azma yake ya kuchangia ujumuishi wa kifedha nchini kupitia huduma za bima, Benki ya NMB Jumatatu wiki hii imezindua msimu wa tatu wa kampeni ya elimu na uelewa wa masuala ya bima ya Umebima jijini Mbeya.

Kama ilivyokuwa kwa misimu ya awali, mchakato wa Umebima wa mwaka huu ni wa kitaifa na lengo lake kuu ni kuunga mkono ajenda ya taifa ya bima kwa wote.

Wakizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika Mwanjelwa-Kabwe, maafisa wa NMB walisema kampeni hiyo inashabiiana na malengo ya serikali ya kuongeza uelewa wa masuala ya bima na kuongeza matumizi ya huduma zake.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Bw. Filbert Mponzi, alisema kwa sasa uelewa wa bima nchini ni mdogo sana na kusisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa kuhakikisha watu wengi zaidi wanakata bima kujikinga na majanga ili kuboresha kiwango cha asilimia 1.6 cha kusambaa kwa huduma hizo.

Aidha, alibainisha kuwa kimsingi kampeni ya Umebima imejikita kuyakabili mapungufu hayo kwa kuuelimisha umma kuhusu umuhimu na faida za bima hasa kwa wale ambao hawajafikiwa na huduma hiyo au kufahamu uwepo wake.

Bw Mponzi alisema tangu NMB ipate leseni ya uwakala wa bima mwaka 2020 imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia kuongeza uelewa wa bima nchini na sasa hivi watu wengi wanazidi kukata bima na kuwa na kinga ya uhakika dhidi ya majanga.

Aliipongeza serikali kwa kuona mbali na kurasimisha utaratibu bunifu wa benki wakala ambao alisema umekuwa na mchango mkubwa katika kufikia malengo ya taifa ya huduma za bima kwa wote.

x

“Sisi kama benki wakala, ni jukumu letu kusaidia ajenda hii ya serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Bima (TIRA) nchini kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanakuwa na uelewa sahihi wa bima na matumizi ya huduma zake,” Bw Mponzi alibainisha.

Kwa mara ya kwanza, kampeni ya Umebima imezinduliwa nje ya Dar es Salaam na Bw Mponzi amesema hilo limefanyika kimkakati kwani kuzinduliwa Mbeya ni sehemu ya kuhakikisha elimu ya bima inasambazwa kote nchini.
Akitolea mfano wa wahanga wa majanga ya moto ya masoko ya Mwanjelwa na Karikaoo, Bw Mponzi alisema mchakato wa Umebima umekuwa na tija kwani watu wengi wanaendelea kunufaika na kuwa na bima za maisha na mali.


“Baada ya kuungua kwa soko la Kariakoo la Dar es Salaam ndani ya wiki moja tuliwasaidia wafanyabiashara waliopoteza mali zao kulipwa fidia ya zaidi ya TZS milioni 400 na mmoja wa wadau wetu wa bima,” alifafanua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Bima, Bw Martine Massawe, alisema NMB ni benki wakala wa makampuni 10 ya bima kama sheria inavyoelekeza.
Kwenye hotuba yake kuzindua kampeni ya Umebima 2023, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw Juma Homera, aliipongeza NMB kwa kuongoza harakati za ukataji bima kupitia uhamasishaji mkubwa wa umma na mtandao wake mpana wa matawi 228 yaliyotapakaa nchi nzima.

“Niwapongeze sana kwa kushirikiana vyema na serikali ya mkoa wa Mbeya na ya Taifa kwa ujumla. Niwahakikishie hili la kampeni la Umebima lina baraka zetu zote kwa hiyo tuendelee kushirikiana katika ujenzi wa taifa,” Bw Homera alisema.

Uzinduzi huo uliudhuriwa pia na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, aliyesema kuwa kampeni ya Umebima ina maana kubwa katika maendeleo ya soko la bima nchini na uelewa wa huduma zinazopatikana ndani yake.

Kupitia kampeni hiyo, Dkt Saqware alifafanua kuwa Benki ya NMB inachangia kikamilifu kutimiza lengo la Mamlaka ya Usimamizi ya Bima la kuongeza uelewa wa huduma za bima kutoka asilimia 37 sasa hivi hadi kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2030 kama Serikali inavyoelekeza.

Leave A Reply