Nuh Mziwanda: Corona Imeturudisha Nyuma Wasanii

KILA kona kwa sasa ni kilio cha virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid 19 ambapo staa wa muziki wa Bongo Fleva, Naftal Mlawa ‘Nuh Mziwanda’ naye anaeleza jinsi wasanii walivyoathirika kwa kipindi hiki.

 

Akibonga na Showbiz Xtra, Nuh alisema Corona imewarudisha nyuma wasanii wengi hasa wa muziki kwani wengi walikuwa wanaishi kwa kutegemea kufanya shoo lakini kwa sasa haiwezekani kwa kuwa mikusanyiko imepigwa marufuku.

 

Aliendelea kusema kuwa pamoja na kutokufanya shoo, pia wamejikuta wakirudi nyuma kimuziki kwa sababu kila mtu anaogopa kuachia kazi mpya kwa kuwa kila kona ni Corona, hivyo wanaogopa kwamba kazi zao zitabuma.

 

Nuh amezungumza mengi, ungana naye hapa chini kwa maswali na majibu zaidi;

SHOWBIZ: Vipi maisha kwa upande wako yakoje kwa kipindi hiki cha janga la Corona?

NUH: Kila kitu kiko poa, kazi zinaendelea vizuri tu, namshukuru Mungu japokuwa wakati huu ni mgumu sana kwa sisi wasanii.

 

SHOWBIZ: Wasanii wengi mlikuwa mnaishi kwa kutegemea kufanya shoo, lakini kwa sasa hamfanyi. Je, mnaendeshaje maisha?

NUH: Ni kweli wasanii wengi walikuwa wanaishi kwa kutegemea shoo lakini kwa upande wangu nilikuwa sitegemei muziki tu bali kutokana na jina langu, kuna biashara nafanya maana nina mtoto anayenitegemea na hii ndiyo inayonisaidia kwa sasa.

 

SHOWBIZ: Je, unatoa ngoma mpya kwa kipindi hiki?

NUH: Nimetoa ngoma mpya tayari na inakwenda kwa jina la Mama Ntilie, niwaombe tu mashabiki zangu wanisapoti.

SHOWBIZ: Kuna ugumu gani katika kutoa ngoma mpya kwa kipindi hiki?

 

NUH: Ugumu upo mkubwa sana maana mitandao ndiyo sehemu kubwa ya kutangaza kazi zetu lakini kwa sasa habari zilizotawala huko ni Corona, hivyo inakuwa ni vigumu kupenya na kutangaza muziki mpya.

 

SHOWBIZ: Kama hivyo ndivyo, umewezaje kujitoa muhanga kwa kuachia ngoma mpya kipindi hiki?

NUH: Nimejiamini na nimemuomba Mwenyezi Mungu kwa sababu watu wamenimisi maana nimekaa kimya muda mrefu, sasa nikiendelea kukaa kimya na hii Corona ndiyo mwanzo wa kusahaulika kabisa, licha ya Corona lazima kazi nyingine ziendelee.

 

SHOWBIZ: Kiujumla Corona imeathiri kazi zenu kwa kiasi gani?

NUH: Corona imeathiri na imetibua kazi nyingi sana za wasanii kwani hata wanamuziki wengine wanahofia kuachia ngoma mpya kwa kuwa wanaona zitabuma.

SHOWBIZ: Unajikingaje na Corona kwa sasa?

 

NUH: Ninatulia ndani, na niwashauri tu watu kwamba wanatakiwa kutulia ndani maana huko nje wanaweza kukutana na mambo mengi, watulie na familia zao na kuzingatia yale yanayotolewa na wizara ya afya.

 

SHOWBIZ: Je, una mpenzi au mchumba?

NUH: Ndiyo, nina mpenzi kwa sababu mimi ni mwanaume niliyekamilika siwezi kukaa bila mpenzi.

SHOWBIZ: Una mpango wa kuoa tena baada ya ile ndoa yako ya kwanza kuvunjika?

 

NUH: Nina mpango na mama yangu anatamani sana kuona nikiwa na mwanamke mmoja anayemjua kwamba ni mkwe wake kwani suala hilo linampa stress sana lakini mpaka sasa sijajua nitaoa lini.

 

SHOWBIZ: Katika muziki wako, mashabiki wategemee nini kikubwa kutoka kwako?

NUH: Wategemee video kali nilizozifanyia Dubai pia ngoma kali nilizofanya kolabo na wanamuziki wakubwa wa nje ya nchi, hivyo naomba wanisapoti kwa hali na mali ili muziki wangu uweze kuendelea mbele zaidi.

MAKALA: MWANDISHI WETU

 

Toa comment