The House of Favourite Newspapers

Nusura Wamasai Watule Nyama-Gabo

0
Gabo Zigamba (wa pili kushoto) akiwa na Wamaasai.

MWIGIZAJI anayekuja juu katika tasnia ya filamu Bongo, Gabo Zigamba, amesema maisha yake ya uigizaji yamejaa kumbukumbu nyingi, lakini moja kati ya vitu ambavyo hatasahau, ni jinsi yeye na wenzake, walivyonusurika kudhuriwa na watu wa jamii ya kimasai.

Gabo, ambaye ni mmoja wa waigizaji wachache wanaodhaniwa kuja kuwa mastaa wakubwa katika filamu nchini, alitoa kauli hiyo alipotakiwa kutaja kitu ambacho hatakisahau katika maisha yake ya uigizaji, kiwe kizuri au kibaya hadi hapo alipo hivi sasa.

 

“Tulikwenda Monduli kutafuta eneo la kushutia filamu ambayo tulitaka kuitumia jamii hiyo, sasa tulivyoingia kwenye kijiji kimoja hivi, ile kusimamisha gari, kwanza walitutazama bila kutusemesha, tulipowafuata wakawa wanatutazama tu na yale majambia yao kiunoni, hawakuonekana kutuogopa, ila walitoa sura kama kututisha.

“Tulipowafikia na kuwasabahi, walikataa kutupa mikono, lakini wazee f’lan hivi walikuwa mbali tukawasikia wakiwasemesha wale jamaa, ndipo mmoja wao aliyekuwa anajua Kiswahili kidogo akatusabahi na kutuuliza tunataka nini.

 

“Tulipowaeleza kuwa nia yetu ilikuwa ni kutaka kufanya nao filamu ya pamoja, aisee, yaani wakazungumza wenyewe kwa wenyewe, tukaona baadhi yao wakitoa majambia yao kama wanataka kutupiga hivi, ikabidi tukimbie kwenye gari kwanza tuwaache waelewane,” alisema Gabo.

Hata hivyo, Gabo alisema baada ya kushindwa kuelewana nao siku hiyo, walilazimika kurejea mjini Arusha na bahati nzuri wakakutana na msichana msomi wa kimasai, Jeniffer Richard ambaye alikwenda kuzungumza na jamii yake ambayo ilimuelewa, ingawa kwa taabu, juu ya nia ya wao kucheza nao filamu.

 

“Baada ya kumpata Jeniffer, ikatubidi pia tumtumie yeye kama msichana wa kimasai, kwanza kuenzi mchango wake hadi Wamasai kutuelewa, lakini pia kwa kuwa alionyesha upeo mkubwa katika ushawishi kwa jamii ile, kiasi kwamba tulidhani atatusaidia sana kuifanya filamu yetu kuwa bora,” alisema msanii huyo ambaye aliitaja filamu hiyo kuwa ni Queen Of Maasai inayotarajiwa kutoka mwishoni mwa mwezi huu.

Stori: Waandishi wetu, Risasi

Leave A Reply