The House of Favourite Newspapers

Nyerere amteua Mzungu kuwa Waziri wa Fedha

0

nyerere Rais wa Awamu ya kwanza, Mwl. Julius Nyerere

ALIKUWA ni mmoja wa Wazungu ambao Waziri Mkuu, Julius Nyerere, alikubaliana nao.  Huyo ni Mwingereza (marehemu) Ernest Albert Vasey aliyekuwa miongoni mwa mawaziri wa mwanzo wa nchi hii baada ya kupata uhuru mwaka 1961.  Alikuwa ni mmoja wa Wazungu waliokuwa wanaunga mkono harakati za  Waafrika kujitawala.

Katika kujenga picha ya kweli kwamba utawala wake usingekuwa wa kibaguzi, Nyerere alihakikisha baraza lake la mawaziri linakuwa na sura pana ya kimataifa, ambapo mbali na mawaziri Waafrika, kulikuwa na mawaziri Wazungu na Wahindi.

Wakati nchi hii inapata uhuru 1961–mwaka ambao MBarack Obama na Uhuru Kenyatta walizaliwa —  Ernest Vasey alikuwa waziri wa fedha, nafasi aliyoendelea nayo hadi mwaka 1962.

Ikumbukwe kwamba wakati wa serikali ya Madaraka, Vasey alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango tangu 1959-1960.

Mwingereza huyo alikuwa mwanasiasa wa kikoloni chini ya himaya ya Uingereza na aliwahi pia kuwa mcheza sinema wakati angali kijana.

Kujiingiza kwake katika siasa kulimfikisha sehemu nyingi duniani hadi Kenya alipofika mwaka 1935 na kupapenda, akaamua kuhamia huko mwaka 1936.

Kwa vile alikuwa na ujuzi wa masuala ya sinema, akajikuta anakuwa meneja wa jengo moja la sinema, jijini Nairobi na baadaye akawa diwani wa eneo la Westland katika Halmashauri ya Manispaa ya Nairobi.

Akiendelea kuimarika katika siasa, hatimaye akawa Meya wa Jiji la Nairobi kati mwaka 1941-1942 na 1944-1946.  Hapo nyuma mwaka 1944,  Vasey akaoa tena (haieleweki nini kilimtokea mke wake wa kwanza aliyemuoa mwaka 1922) ambapo mwaka 1945 alitunukiwa medali ya Malkia ya Companion of the Order of St Michael and St George (CMG) iliyomfanya aanze kuitwa Sir Ernest Vasey.

Hata hivyo, mwaka 1962, Vasey alijiuzulu uwaziri huo aliopewa na Nyerere kutokana na chuki ya wanachama wa chama tawala wakati huo cha Tanganyika African National Union (TANU) ambao hawakupenda nafasi hiyo nyeti na muhimu kuwa mikononi mwa mtu kutoka nchi za nje.  Hivyo, alijiuzulu na kumwachia nafasi hiyo Mwafrika, lakini akakubali cheo cha Mshauri Mkuu wa Masuala ya Fedha wa Tanganyika, lakini akiendelea kupata mshahara uleule wa uwaziri hadi mwaka 1966.

Baadaye akafanya kazi za masuala ya fedha huko Pakistan kwa miezi kadhaa na kurejea Kenya na kujikita katika masuala ya uigizaji hadi kifo kilipomfika.

Ni Ernest Albert Vasey aliyezaliwa Maryport, Cumberland, Uingereza mwaka 1901 na kufariki mwaka 1984 akiwa ameacha watoto wawili wa kiume katika kila moja ya ndoa zake mbili.

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: Global TV Online

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE:@shigongotz

Leave A Reply