The House of Favourite Newspapers

Nyerere, Kawawa wakimbilia Kigamboni

0

Nyerere, KawawaLEO hii jambo hili likisimuliwa ni kama hadithi! Lakini si hadhithi. Lilitokea miaka ipatayo 52 iliyopita, wakati wasomaji wengi wa safu hii walikuwa hawajazaliwa na waliolishuhudia walikuwa ama watoto wadogo au vijana ambao hivi sasa wengi wao ni wazee wa zaidi ya miaka 60.

Ni uasi wa jeshi la ulinzi la Tanganyika (wakati huo) likiitwa Tanganyika Rifles ulioanzia Kambi ya Colito Barracks ambayo leo inaitwa Lugalo, ya jijini Dar es Salaam mnamo Januari 1964. Walioshuhudia tukio hilo – hususan waliokuwa wakiishi Dar es Salaam – watakumbuka vurugu kubwa iliyozuka katika jiji hilo ambapo watu waliuawa na mali zikaporwa na askari wa jeshi hilo hususan sehemu za Magomeni na katikati ya Jiji la Dar.

Watu wachache sana wanaolifahamu tukio hilo ambalo hata vyombo vya habari huwa havilitaji sana. Lilitokea miaka ipatayo mitatu baada ya Tanganyika kupata uhuru Desemba 9, 1961 na siku nane baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Tukio hilo ambalo lilijaza askari wakiwa na silaha mbalimbali mitaani lilidaiwa lilikuwa la kuibana serikali iwaondoe maofisa wazungu jeshini,  iwapandishe vyeo askari Waafrika na iboreshe hali ya maisha jeshini.

Uasi huo uliofanyika pia kwa wakati mmoja huko Kenya na Uganda, nchi zilizokuwa zikitawaliwa na Uingereza, kwa nchini ulisambaa katika vikosi vingine vya jeshi mikoani kuwaunga mkono wenzao wa Dar.

Hivyo, wachambuzi wengine walisema uasi huo ulikuwa na nia  ya wanajeshi kuziangusha serikali za nchi hizi.

Wakati wa uasi huo, aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Julius Nyerere na makamu wake, Rashid Kawawa, waliikimbia ikulu ambacho mashuhuda husema walitoroshwa kutoka ikulu katika teksi moja wakiwa wamevishwa mabaibui na kwenda kujificha Kigamboni.

Kiongozi aliyebaki mitaani wakati wa vurugu hizo kubwa zilizochukua muda wa siku zipatazo nne, alikuwa ni waziri wa ulinzi, Oscar Kambona,  ambaye wanajeshi walionekana kumkubali kuwasiliana naye.

 Kwa kifupi, uasi huo ulizimwa na wanajeshi wa Uingereza baada ya Nyerere kuiomba Uingereza imsaidie. Meli ya kivita ya Uingereza iliyokuwa ikiitwa HMS Centaur ikiwa Aden, Somalia, ilifika Dar siku ya nne baadaye ikauzima kirahisi uasi huo.

Helikopta kadhaa zilizokuwa katika meli hiyo ziliibuka juu zikiwa zimening’iniza magari ya Land Rover na kwenda kutua kambi ya Lugalo yakifuatiwa na askari ambao waliivamia kambi hiyo na kuwasambaratisha kirahisi askari waasi.

Askari hao walikimbilia mitaani na vichakani wakitupa silaha na magwanda yao, waliobaki walikamatwa.  Huo ndiyo ukawa mwisho wa uasi huo, na askari wa Uingereza wakachukua nafasi yao kwani jeshi hilo la Tanganyika Rifles lilivunjwa baada ya Nyerere kutoka mafichoni.

Baada ya muda, Nyerere aliomba msaada wa askari kutoka Nigeria ambao walikuja kuchukua nafasi ya askari waliofukuzwa.  Askari hao wa Nigeria walisambazwa sehemu mbalimbali nchini.

Kwa “vijana wa zamani” waliokuwa Shinyanga, watakumbuka kuwaona askari hao waliokuwa wameweka kambi huko Old Shinyanga!

***Mwisho***

Leave A Reply