POLISI wa Migori, Jimbo la Nyanza Kusini mwa Kenya, wamesema wamepata nyeti za mwanaume aliyejulikana kwa jina la Felix Otieno (31) aliyevamiwa na watu wasiojulikana kisha kunyofolewa mnamo Aprili 13, mwaka huu katika eneo la Suna Magharibi.
Mkuu wa Polisi wa Migori, Joseph Nthenge amewaeleza wanahabari kwamba nyeti za Felix Otieno zilipatikana mjini Sirare, Tanzania usiku wa Jumatano baada ya kuarifiwa na wakazi wa eneo hilo.
Nthenge alisema kwamba, maafisa wa usalama wanamfuatilia mmoja wa watuhumiwa waliomvamia Felix, ambaye anadaiwa baada ya kugundua kwamba anasakwa, aliamua kuzitelekeza nyeti hizo zikiwa ndani ya mfuko wa plastiki na kukimbilia kusikojulikana.
Kwa mujibu wa Nthenge, nyeti hizo zilipelekwa katika Hospitali Kuu ya Migori huku Felix akizidi kuuguza majeraha katika Hospitali Kuu ya Kisii ambako madaktari wanasema afya yake imezidi kuimarika.
Aidha, chifu wa Kata ndogo ya Mukuro, alisema mwathiriwa alipovamiwa alikuwa pamoja na rafiki yake ambaye alifanikiwa kuwakimbia watu hao na kukwepa unyama huo. Inasemakana, Felix alidungwa sindano mara kadhaa na wahalifu hao kabla ya kunyofolewa nyeti zake na kutokomea nazo.
Comments are closed.