Nyoni: Acheni Presha, JS Saoura Watafungika

BAADA ya kupata majeraha ambayo yatamfanya aukose mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kiraka wa Simba, Erasto Nyoni amewaambia mashabiki wa timu hiyo wasiwe na presha kwani kwa jeshi lililopo anaamini bado JS Saoura ya Algeria watafungika.

 

Nyoni ambaye ni mmoja wa mabeki bora ndani ya kikosi cha Simba, alipata majeraha ya goti wakati akiitumikia timu hiyo kwenye michuano ya Mapinduzi Visiwani Zanzibar. Kutokana na majeraha hayo, Nyoni atakaa nje kwa wiki tatu.

 

Kiraka huyo ameliambia Championi Jumatano, kuwa licha ya yeye kuumia na kuukosa mchezo huo wa kimataifa lakini hana hofu hata kidogo kwa sababu wachezaji wenzake ambao wamebaki wanaweza kuwamaliza Waarabu.

 

“Sijisikii vizuri kupata majeraha haya ambayo yananifanya niukose mchezo huu wa kimataifa, lakini hakuna namna kwa sababu tayari imeshatokea na sitakuwepo.

 

“Lakini niwaambie watu kwamba wasiwe na hofu kutokuwepo kwa kuwa nafahamu wachezaji wenzangu wanaweza kuwachinja Waarabu.

 

“Kikubwa namuomba Mungu nipone haraka na niwaambie mashabiki wajitokeze uwanjani kwenye mechi yetu hiyo wakawape sapoti ya kutosha wachezaji,” alisema Nyoni ambaye aliwahi kucheza Vital’O ya Burundi.

 

Simba itacheza mechi yake ya kwanza ya Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria katika Uwanja wa Taifa jijini Dar, Jumamosi hii.

Stori na Said Ally,

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Toa comment