Nyoni Kubeba Mikoba ya Juuko Murshid

IPO wazi kwamba beki Juuko Murshid hatocheza mechi ya kimataifa dhidi ya JS Saoura kutokana na kuwa na kadi za njano, sasa beki Erasto Nyoni rasmi atabeba mikoba yake.

 

Nyoni ambaye ni kiraka alikuwa nje ya uwanja akiuguza kifundo cha mguu alichoumia kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu. Hivyo kutokana na maendeleo yake, Machi 9, mwaka huu, anaweza kuwa sehemu ya nyota watakaocheza mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya JS Saoura ya Algeria.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Nyoni alisema kuwa, kwa sasa yuko fiti na anauhakika na afya yake, hivyo kama hakutatokea kikwazo kipya basi atakuwa ni miongoni mwa wachezaji katika michezo ijayo na ataambatana na Simba kwenda Algeria.

 

“Kusema kweli kwa sasa nipo fiti, madaktari wamenithibitishia hivyo, bila shaka naamini endapo hakutatokea chochote basi nitakuwa tayari kuwa sehemu ya michezo yetu ijayo na hata ule wa marudiano dhidi ya JS Saoura nchini Algeria.

 

“Kikubwa naendelea kumuomba Mungu anipe uzima zaidi kwani tangu nimeanza mazoezi kila mmoja anaridhishwa na mwenendo wangu hii ni kwa wachezaji wenzangu, makocha na daktari kwa ujumla wao tayari wameshanipa baraka zao,” alisema Nyoni.

MUSA MATEJA

Toa comment