Nyuma ya BSS kuna damu, machozi na jasho!
“Vipi, nikuwashie AC? Naona kama unahisi joto, kuwa huru hapa ni mahali ambapo mtu akifika, uhuru wa nafsi na akili unahitajika sana, pia karibu kwa vinywaji, niambie tu chochote, nitakuhudumia,” ni mazungumzo ya kwanza kabisa kutoka kinywani mwa mwanamke shujaa, hodari, jasiri na mpambanaji katika maisha.
Staili ya maisha yake, ni kawaida tofauti na hadhi ya jina lake katika jamii! Hajikwezi wala kujibagua na watu wa kawaida, hajali sana umaarufu alionao, ingawa kutoka moyoni, nikiri kuwa mwanamke huyu ni maarufu na heshima yake kwenye jamii ni kubwa.
Huyu si mwingine, bali ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Benchmark Productions na muasisi wa shindano la kusaka vipaji kwa njia ya uimbaji la Bongo Star Search (BSS), Ritha Paulsen ‘Madam Ritha’.
Ni ndani ya jumba kubwa lenye hadhi, zilipo ofisi za kampuni hiyo, Mikocheni jijini Dar. Nikiwa nimeketi na kuufaidi uzuri wa ofisi hiyo, iliyonakshiwa kwa samani za thamani ya juu. Mkononi nikiwa na kalamu, kifaa maalum cha kurekodia pamoja na kijitabu cha kumbukumbu (Diary), yote ni kuhakikisha kila anachokisema mwanamke huyo shujaa, kinanakiliwa kwa ufasaha.
“Aaah, hapana, niko sawa na kwa vinywaji nitakuambia muda ukifika, asante sana Madam,” namjibu kwa utulivu huku nikilitazama jokofu (friji) lililomo ofisini hapo, ambalo liliashiria kusheheni aina mbalimbali za vinywaji.
Ndiyo, lengo ni moja tu. Kujua safari nzima ya maisha yake na kwa namna gani aliweza kufika hapo alipo kimaisha, akiwa kama mwanamke na kufanikiwa kuwa faida kwa taifa kwa kuibua vipaji, kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa taifa kupitia shindano lake, BSS.
“Unataka kujua nini hasa kutoka kwangu?,” ananiuliza huku akivua miwani na kunikazia macho bila kuyapepesa, nami moyoni najawa na hisia kali, hisia za kuandika kwa weledi wa hali ya juu.
“Mimi na wasomaji wangu tunataka kujua safari nzima ya maisha yako, tangu kuzaliwa hadi sasa, ukiwa kama mwanamke ambaye naamini ulikulia katika zama ambazo mwanamke alionekana si chochote kwa jamii, kutokana na umri wako, ni namna gani mtu hususan mwanamke anayetamani kuwa kama wewe, afanye ili aweze kuwa hivyo,” naeleza kwa ujasiri na kumfanya atabasamu kwa muda huku akiniangalia kuanzia kichwani hadi miguuni.
“Safari yangu ya maisha si ya kufurahisha sana, niko hivi nilivyo, baada ya kuumia kwa kiwango kisichotamkwa, kwa mtu akiniangalia kwa sasa, si rahisi kabisa kuamini kama mapito yangu yanakatisha tamaa, lakini huo ndiyo ukweli, siku zote njia ya kuelekea kwenye utukufu huwa siyo nzuri sana,” anasema Madam Ritha.
Wakati mazungumzo yakiendelea, ghafla mlango unafunguliwa na anaingia msichana mrembo, mrefu, mwembamba mwenye muonekano wa kishombeshombe akiwa na sinia lililobeba kahawa, vitafunwa mbalimbali na vikombe viwili.
Baada ya kumaliza jukumu lake, anaondoka na kutuacha wawili, mazungumzo yanaendelea…..
“Karibu, ilibidi nimwagize msichana wangu vitu hivi kwa njia ya SMS, maana nilihisi unaona aibu kuagiza vinywaji, haya karibu na tuendelee na mazungumzo,” anasema Madam Ritha huku akinisogezea kikombe cha kahawa, mazungumzo yakaendelea kama kawaida.
“Kabla sijaanza rasmi kusimulia safari ya maisha yangu ambayo kwa hakika imejaa maumivu makali, kwanza nataka kuwaasa watu wa rika zote kuwa, mafanikio ya kweli maishani, kamwe hayaji kwa njia rahisi, na kuna siri moja ambayo wengi hawaijui katika maisha,” anasema na kukohoa kidogo.
Je nini kiliendelea.
Hii ni simulizi nzuri ya kusisimua ambayo itakufundisha na kukutia moyo katika kila hatua ngumu unayopitia.
Tukutane Jumamosi kwenye gazeti hili kwa muendelezo.
JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!