Nyumba ya mjane Chiku Juma Athuman iliyopo Kinondoni Studio jijini Dar es Salaam, imebomolewa kufuatia kuibuka kwa mgogoro wa utata juu ya umiliki wake, baada ya mtu mwingine kuibuka na kudai kuwa na hati ya umiliki wa eneo hilo.
Baadhi ya wanafamilia wa familia ya mjane huo, wamesema nyumba ya familia imebomolewa na mtu waliyemtaja kwa jina moja la Malugu, ambaye alifika na watu wanaodaiwa kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi na kubomoa nyumba hiyo kwa nguvu, wakiwaacha wanafamilia wakikosa cha kufanya.
Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa wanafamilia hao aliyejitambulisha kwa jina la Hawa Issa, alisema wanailalamikia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayoongozwa na William Lukuvi kwa kushindwa kutenda haki kwa kutoa hati mbili kwa watu wawili tofauti na kusababisha upande mmoja kutumia nguvu na kubomoa nyumba yao.
Hawa amemuomba Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati ili waweze kupata haki yao, kwani wanayo hati ya umiliki wa nyumba hiyo.
Mjumbe wa Mtaa huo, Nassor Ramadhani, akizungumza na Mtandao wa Global Publishers, amesema anasikitishwa na kitendo kilichofanywa na Malugu kwani hakufata taratibu za kisheria za uvunjaji nyumba.
“Ilitakiwa wanafamilia wapewa taarifa ya maandishi ya muda wa wiki moja au mwezi ili kuwawezesha kuondoa mali zao lakini hakufanya hivyo, huu ni uvunjaji wa sheria,” alisema.
NA DENIS MTIMA/GPL
Comments are closed.