The House of Favourite Newspapers

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Kuzinduliwa Leo

Mastaa Watembelea Shinda Nyumba (15)DAR ES SALAAM: Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini, Tarimba Abbas Tarimba ndiye atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa shindano la Shinda Nyumba Awamu ya Pili, utakaofanyika katika ofisi za Global Publishers zilizopo Bamaga-Mwenge jijini Dar leo Jumatano.

Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho amethibitisha kuwa, Tarimba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, ndiye atakayekata utepe kuzindua shindano hilo kubwa ambalo mshindi wa jumla, atajishindia zawadi ya nyumba yenye thamani ya mamilioni ya shilingi iliyojengwa jijini Dar.

Nyumba (8)Hii ni mara ya pili kwa Kampuni ya Global Publishers kufanya shindano hilo ndani ya mwaka mmoja na hivyo kuifanya kuwa taasisi pekee miongoni mwa vyombo vya habari kutoa zawadi kubwa ya nyumba kwa wasomaji wa magazeti yake ambayo ni Championi, Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi na Amani.

“Kila kitu sasa kimekamilika, iliyobaki ni kusubiri siku tu ambayo ni  kesho Jumatano, Mkurugenzi Tarimba amekubali kuwa mgeni rasmi na kwa sababu hiyo, kazi sasa imekwisha. Nitoe wito tu kwa wasomaji wetu, hii ni fursa nyingine nzuri kwao kuweza kupata chochote kutoka kwetu, kama ninavyosema mara kwa mara, Global Publishers inawathamini wasomaji wake na inatambua mchango wao katika kuifanya kampuni kufikia hapa ilipo leo.

“Tumekuwa kampuni namba moja ya magazeti pendwa na michezo kutokana na wao kutuunga mkono kwa miaka yote, kwa kutambua hilo, ndiyo maana tunatoa zawadi hii ili na wao wajione ni sehemu ya Global Publishers, nichukue nafasi hii kuwaomba wanunue magazeti yetu ili wawe katika nafasi nzuri ya kuibuka mshindi, kwa sababu kadiri unavyopata kuponi nyingi ndivyo unavyokaribia kuibuka mshindi,” alisema Mrisho.

Mastaa Watembelea Shinda Nyumba (16)Licha ya mshindi wa kwanza kujipatia nyumba, pia zawadi ndogondogo zimeboreshwa na kuongezwa. Zawadi ya pikipiki itatolewa kila mwezi, kwa miezi yote ambayo shindano hilo litafanyika tofauti na shindano lililopita, pia zitatolewa televisheni kubwa na za kisasa, simu za kileo, vyombo vya nyumbani, fulana, kofia na vitu vingine vingi vidogovidogo.

Katika shindano la mwaka jana, mshindi wa nyumba kubwa na ya kisasa, iliyojengwa Mbezi-Salasala nje kidogo ya Jiji la Dar, alikuwa ni Nelly Mwangosi, mama wa watoto wawili, ambaye pia ni mjasiriamali, mwenyeji wa mkoani Iringa. Aliposhinda nyumba hiyo, ndani aliikuta ikiwa na samani zake zote.

“Pamoja na kwamba nilishinda mwaka jana, mwaka huu pia nitashiriki kama kawaida, lakini kikubwa zaidi ni kwamba nimewaambia ndugu zangu wote tushiriki, kwa sababu huwezi kujua, mimi sikujua kama nitashinda mwaka jana. Wao wameniambia lazima washiriki kwa kusoma magazeti yote yenye hizo kuponi,” alisema Nelly, alipotembelewa na timu ya waandishi kutoka Kampuni ya Global Publishers nyumbani hapo hivi karibuni.

 

Comments are closed.