The House of Favourite Newspapers

NYUMBA YA URITHI YAZUA BALAA

MSONDO Ngoma Music Band waliona mbali walipotoa wimbo wa Kilio cha Mtu Mzima, ambapo mashairi yake yanasema hivi:  “Tunatoana roho Yarabiii, kwa mali alizoacha baaba…” Na kweli nyumba ya urithi imezua balaa jijini Dar es Salaam ambapo juzikati maeneo ya Kijitonyama watoto wa baba mmoja kudaiwa kugombea mali alizoacha marehemu baba yao, Omary Mkuruzo aliyefariki dunia mwaka 2014.

Awali, Risasi Mchanganyiko lilipigiwa simu majira ya mchana na kupewa taarifa kwamba kuna ugomvi mkubwa wa kifamilia umetokea maeneo hayo ambapo watu wamefika na kutoa vyombo vya jirani yao nje. “Mwenye nyumba hayupo, lakini kuna watu wamefika na kuvipakia vyombo vyake kwenye gari na wanataka kuondoka navyo,” chanzo kililiambia Risasi Mchanganyiko kwa njia ya simu.

Kwa kuwa eneo hilo si mbali sana na ofisi za Global Publishers zilizopo Sinza-Mori, mwandishi wetu alitumia dakika chache kufika na kushuhudia umati mkubwa wa watu wakiwa eneo hilo huku gari lililobeba vyombo likiwa chini ya ulinzi mkali wa majirani. Moja kwa moja, Risasi Mchanganyiko lilianza kuzungumza na Saida Omary mtoto wa marehemu kwa mke mdogo ambaye alikuwa na haya ya kusema:

“Watoto wa marehemu tupo nane, kwa mama mkubwa (mke mkubwa wa marehemu) kuna wenzetu wanne. “Wenzetu wanaishi Sinza na sisi tupo Kijitonyama pamoja na mama yetu, lakini siku za hivi karibuni kumetokea mgogoro kati yetu, ambapo wenzetu wanataka tutoke kwenye hii nyumba,” alisema Saida.

Aliongeza kuwa, siku hiyo ya tukio baadhi ya ndugu zao walifika kwenye nyumba hiyo wakiwa na gari kwa lengo la kuhamisha vyombo vyao kama njia ya kuwatoa kwenye hiyo nyumba. Hata hivyo, zoezi hilo halikuwezekana kutokana na majirani kulizuia gari hilo lisiondoke na kisha polisi kuitwa ili kuingilia kati sakata hilo.

MAMA’KE SAIDA ANENA

“Mimi ni mke mdogo wa marehemu, nilikuwa nikiishi na mume wangu hapa na tumejenga wote hii nyumba, lakini cha kushangaza hawa watoto wa bi’mkubwa wangu ndiyo hawanitaki, wanataka mimi niondoke kwenye hii nyumba.

“Najiuliza na huu uzee wangu nitaenda kuishi wapi na huyu binti yangu (Saida) maana niko naye hapa? Naomba serikali inisaidie, nanyanyaswa sana,” alisema mama huyo aitwaye Amina Hamza.

MTUHUMIWA ANENA

Mmoja kati ya watoto wanaotuhumiwa kuvunja mlango wa mke mdogo wa marehemu na kutoa vyombo ndani aitwaye Kibwana alisema, walikuwa na barua (hakusema inatoka mamlaka gani) iliyowaruhusu kufanya hivyo.

“Mimi ni mmoja wa watoto wa marehemu Mkuruzo, baada ya marehemu mzee kufariki tulifanya kikao cha kifamilia ikaamuriwa kuwa mdogo wangu mimi aitwaye Salum Mkuruza ndiyo awe msimamizi wa mirathi, tukaamua kwenye nyumba ya Kijitonyama badala ya kukaa wanandugu tuipangishe, kisha kodi tuwe tunagawana, kwa sababu hata marehemu mzee naye alipenda iwe hivyo kabla hajafa.

“Sasa tunashangaa kwamba tulishakubaliana iwe hivyo, lakini dada yetu huyu mdogo (Saida) hataki, kuna mpangaji alihama ndipo na yeye akaja kuishi hapa na mama yake kinyume na utaratibu tuliokubaliana.

“Leo hii tumekuja kutoa vyombo na broka wa mahakama ambaye ndiyo alikuwa anatekeleza amri ya mahakama. Kwa hiyo, inatakiwa aondoke hapa nyumbani na chumba alichokuwa akiishi yeye kitapangishwa,” alisema Kibwana.

JIRANI AZUNGUMZA

Mmoja kati ya majirani wa familia hiyo iliyotolewa vyombo nje aliyejitambulisha kwa jina moja la Zuhura alisema kuwa anaifahamu familia hiyo kwa miaka mingi ndiyo maana alikerwa na kitendo cha kuja kuchukuliwa vyombo vyao wakati wenyewe hawapo.

“Nilihamia hapa mwaka 1986, nikawakuta hapa huyu mama na mumewe. Kwa hiyo naifahamu sana familia hii. Nilishangaa kuona vyombo vinatolewa nje, nilipouliza wakashindwa kunyoosha maneno, ikabidi tulizuie gari lisiondoke,” alisema Zuhura.

MJUMBE NAYE AZUNGUMZA

Mjumbe wa mtaa, Ndangula Ismail naye alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kwamba sheria ichukue mkondo wake kwa sababu watuhumiwa hawakufuata utaratibu. “Marehemu alikuwa ni rafiki yangu na alikuwa na nyumba mbili na wanawake wawili, mmoja alikuwa akiishi naye Sinza na mwingine alikuwa akiishi hapa Kijitonyama.

GARI LAPELEKWA POLISI

Baada ya sakata hilo kuingiliwa na jeshi la polisi, gari lililokuja kuchukua vyomba vya familia ya Amina liliamriwa kupelekwa kituo cha polisi Mabatini kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Hata hivyo, habari zilizopatika baadaye zilieleza kuwa jeshi hilo liliagiza watuhumiwa kurejesha vitu walivyokuwa wamechukua huku likipiga marufuku watuhumiwa hao kukanyaga kwenye nyumba hiyo hadi mahakama itakapomaliza shauri la msingi la kugawa mirathi kwa wafiwa

STORI: MEMORISE RICHARD, RISASI

Comments are closed.