Nyumba za Yamoto Siri Nzito Yafichuka, Fela Ahitaji Sapoti!

Eneo la mbele la Nyumba za Yamoto Band zilizopo Mbande-Kisewe jijini Dar.

KATIKA Muziki wa Bongo Fleva, kuna wadau wengi ambao wamekuwa wakijitolea kwa hali na mali kila kukicha katika kuwaunga mkono vijana wenye vipaji hasa vya ku-rap na kuimba ili waweze kufikia ndoto zao. Wadau hawa wanaweza kuwa mtu mmojammoja, kundi, bendi au taasisi ambazo huanzishwa kwa mlengo huo.

Lakini pia wapo wadau wengine ambao wamekuwa wakijitolea tangu Bongo Fleva imeanza kutamba, ukiachana na bendi za vijana wadogo kama Skylight, La Musica, Vijana Classic, Ruby Band na taasisi zingine kama THT na Mkubwa na Wanawe.

Mlinzi wa nyumba za Yamoto Band, Hussein Mpili akitoa maelezo ya nyumba hizo kwa waandishi.

Mkubwa na Wanawe ni kituo kilichoanzishwa na mdau maarufu kwenye tasnia ya muziki nchini, Said Fella ‘Mkubwa Fella’, ambaye aliwahi kuwa mmiliki wa Kundi la TMK Wanaume kabla halijaparanganyika na kutengeneza makundi mawili ya TMK Wanaume Halisi na TMK Wanaume Family kufuatia baadhi ya wasanii wake kujitoa kundini akiwemo Juma Nature na KR Mullah.

Mbali na wasanii hao kujitoa, Fella pamoja na mambo mengine mengi ni miongoni mwa wadau ambao wamekuwa wakisimamia kile wanachokiamini katika kuwatimizia vijana ndoto zao, amekuwa chachu ya mafanikio ya wasanii wengi wenye ndoto za kufika mbali kimuziki.

Aliyekuwa Meneja wa Kundi la Yamoto Band Said Fella ‘Mkubwa Fella’.

Huwezi kuyataja mafanikio ya Chegge, Juma Nature, Mhe. Temba na Stiko kwa mfano, bila kutambua umuhimu wa Said Fella kwani mbali na kuwaunga mkono kwenye kazi, pia ameweza kuwajengea nyumba kila mmoja!

Huyo ndiye Fella ambaye alipoanzisha kituo cha Mkubwa na Wanawe ambacho kwa sasa kina wasanii zaidi ya 70 akiwemo Dulla Makabila na Kayumba, aliamua kuibua vijana wanne ambao walikuwa ndani ya kituo hicho waliotengeneza Bendi ya Yamoto. Vijana hao ni Dogo Aslay, Maromboso, Becka One na Enock Bella.

Muonekano wa ndani katika moja ya nyumba hizo.

Katika ubora wao, Yamoto Band ilitusua na ngoma kibao zikiwemo Yamoto, Bora Kijijini, Basi na Mama. Mbali na kutamba na nyimbo hizo bendi hii imevuruga kwa shoo ndani na nje ya Bongo, kifupi ilikuwa gumzo kutokana na vijana wachanga kwenye ‘gemu’ kujizolea umaarufu ndani ya muda mfupi.

Nyumba ya Msanii Kayumba (kushoto yenye paa)

Kwa sasa bendi hiyo haionekani mara kwa mara japo kwenye matukio makubwa ya kiburudani, hutokea ikiwa na wasanii hao. Kwa mujibu wa Fella mwenyewe ambaye ndiye mwanzilishi anasema bendi hiyo haijafa, malengo yake yalikuwa ni kuwainua vijana hao waweze kujisaidia na kuwasaidia wengine na kwamba wakifika mahali kila mmoja awe na uwezo wa kufanya kazi peke yake.

Ndiyo maana amemuachia Maromboso na Becka waende kwenye lebo zingine ili waendelee na kazi zao za kimuziki lakini uongozi wa Yamoto unabaki palepale ukisimamia kazi pale watakapofanya kazi kama kundi.

Muonekano wa juu katika moja ya nyumba hizo.

Hata hivyo mbali na sintofahamu hiyo katika ubora wao, miongoni mwa mafanikio ambayo ‘madogo’ wa Yamoto waliyavuna ni kila mmoja kujengewa nyumba maeneo ya Mbande-Kisewe jijini Dar.

Ni Fella ndiye alizitambulisha nyumba hizo mbele ya waandishi wa habari mwaka jana. Ambapo tangu azitambulishe, kumekuwa na ‘ukakasi’ juu ya kinachoendelelea huku wengine wakitupa lawama bila kujua sababu zilizo nyuma ya pazia.

Kwa mujibu wa mlinzi anayelinda kwenye nyumba hizo, Hussein Mpili, akizungumza na Showbiz ya Ijumaa, amesema tangu Fella aende na waandishi wa habari, amekuwa karibu na nyumba hizo japokuwa ujenzi umesimama kwa muda kutokana na mzunguko wa kiuchumi kuwa mbaya.

Baada ya Showbiz kubaini kinachoendelea kwenye nyumba hizo, ambazo bado zinahitaji matengenezo kwa kiasi kikubwa hasa katika kumalizia ndani, iliamua kumtafuta mkubwa Fella na kuweza kumbana ili afunguke ukweli juu ya nini kilichojificha kwenye suala la nyumba hizo na kubaini siri nzito;

Showbiz: Mkubwa nini kinaendelea kwenye nyumba za Yamoto, inasemekana umezitelekeza, mara ni vijana ndio hawazitaki, ukweli ni upi?

Muonekano wa nyuma ya nyumba hizo.

Fella: Ni nani anayeweza kujenga nyumba na kuzitelekeza? Nyumba hazijatelekezwa zipo.

Showbiz: Vipi ujenzi, mbona umesimama tena na hawajakabidhiwa hadi leo au kundi limeshakufa?

Fella: Bado marekebisho hayajamalizika ili niwakabidhi. Kundi la Yamoto haliwezi kufa. Kuhusu nyumba hata kama hao vijana wakiwa nje ya Yamoto, nyumba zitabaki kuwa mali yao kwa sababu niliwajengea wao. Kwani si nilikuwa ninamiliki kundi la TMK, leo sipo na Nature, Temba na Chegge sipo na Stiko, lakini mbona wote niliwajengea nyumba na sikumnyang’anya hata mmoja?

Mlinzi akimpa maelekezo mwandishi

Showbiz: Tatizo hasa lipo wapi mpaka sasa hawajakabidhiwa?

Fella: Nahitaji niwakabidhi nyumba ambazo zipo kamili, zinahitaji marekebisho ni kwa sababu tu hali ya mzunguko wa kiuchumi siyo nzuri kwa sasa ndiyo maana nimeganda. Kumbuka nimekuwa mdau pekee ninayemiliki kituo cha kusaidia vijana chenye vijana zaidi ya 70 na wote wananiangalia kila siku kuanzia kula, kuvaa, kusoma na hadi vipaji vyao. Wakati mwingine naelemewa, kwa hiyo kama kuna wadau ambao wanaweza kujitokeza na kusaidia kukamilisha ujenzi nipo tayari na hata kama wapo wanaoweza kutia mkono katika kituo changu ili tuwasaidie vijana hawa, pia nipo tayari maana mzigo ni mzito, nahitaji sapoti ya wadau wengine pia.

KUTOKA SHOWBIZ

Tunawaomba wadau na wafuatiliaji wa karibu katika masuala ya burudani kujitokeza kwa wingi kumsaidia mdau Fella katika kuendesha kituo na kuwasaidia wasanii zaidi ya 70. Anachofanya ni cha kuigwa na kutiwa moyo.

IMEANDALIWA NA BONIPHACE NGUMIJE, ANDREW CARLOS, IRENE MNYITAFU NA ALLY KATALAMBULA.


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Loading...

Toa comment