OFISA TRA ANAYETUHUMIWA KUMILIKI MAGARI 19, ALIANZA KAZI AKIWA NAYO
Ofisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi ( wa pili mbele) anayetuhumiwa kumiliki magari 19 yenye thamani ya Shilingi Milioni 197.6 akishuka ngazi za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kusikiliza kesi inayomkabili.
Ofisa Mchunguzi wa TRA, Tumaini Fadhili, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Ofisa Msaidizi wa Forodha wa mamlaka hiyo, Jennifer Mushi, anayekabiliwa na kesi ya kumiliki magari 19 yenye thamani ya Shilingi Milioni 197.6 aliajiriwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akiwa na mali zake.
Ofisa huyo ameeleza hayo leo wakati akiongozwa na wakili wa Jennifer, Fulgence Masawe, alipotoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Akitoa ushahidi wake, Fadhili amedai yeye ni mchunguzi wa ndani wa TRA, huku majukumu yake yakiwa ni kufanya uchunguzi wa malalamiko yote na kuhakiki mali za watumishi ili kudhibiti vitendo vya rushwa.
Alipoulizwa na wakili huyo kwamba anamfahamu Jennifer, alijibu kuwa anamfahamu kwa sababu aliwahi kumchunguza.
Pia aliulizwa kama anafamu idadi ya mali za Jennifer na thamani yake, Tumaini alijibu anafahamu na alipouliza alianza alianza kazi lini TRA, alijibu kuwa ni tangu mwaka 2010, lakini awali aliajiriwa katika sekta binafsi.
Vilevile aliulizwa iwapo Jennifer aliajiriwa TRA akiwa na mali zake, Fadhili alijibu ndiyo ambapo alipoulizwa alitumia mfumo gani kubaini idadi ya magari ya Jennifer, alidai kuwa alitumia mfumo wa usajili wa magari lakini hakuwahi kuyaona kwa macho.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Peter Vitalis, alimuuliza Fadhili ni mali gani ambazo Jennifer anamiliki, alidai kuwa ni zaidi ya magari 10 na waliyabaini kwa sababu alishindwa kuorodhesha vitu hivyo.
Baada ya kutolewa ushahidi huo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 16,mwaka huu.
Jennifer anakabiliwa na kosa la kumiliki magari 19 ambayo anadaiwa aliyaingiza nchini kutokea Japan yakiwa na thamani ya shilingi Milioni 197,601, 207.
Comments are closed.