The House of Favourite Newspapers

Okwi Awaaibisha Waarabu Uturuki, Video Ya Bao Lake Ipo Hapa

Mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi.

EMMANUEL Okwi jana Jumamosi alifunga mabao mawili na kuipa ushindi wa kwanza Simba tangu ilipotua Uturuki wiki mbili zilizopita.

 

Okwi alifunga mabao hayo dhidi ya mabingwa wa Palestina, FCE Ksaifa huku lingine likifungwa na Meddie Kagere na kuifanya Simba ishinde mabao 3-1 katika mchezo mkali uliopigwa Uwanja wa Hoteli ya Green Park mjini Kartepe Kocael.

 

Huu ni mchezo wa pili kwa Simba tangu ilipotua Uturuki kuweka kambi ambapo mechi ya kwanza walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Moulodia Oujda ya Morocco.

 

MARUFUKU USWAHILINI

KWA taarifa yako shabiki wa Simba popote ulipo, wachezaji wakikanyaga tu Dar es Salaam kesho Jumatatu alfajiri hawataonekana uswahilini. Matajiri wa Simba wameamua watakwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Serena ambayo wanakaa wageni wa kishuwa tu.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alithibitisha kwamba; “Ratiba imebadilika badala ya kutua Jumapili alfajiri itafika Jumatatu alfajiri hapa nchini na kuendelea na maandalizi pamoja na shughuli zile za kijamii ambazo tunafanya kuelekea siku maalum ya Simba day.”

 

Wachezaji hao ambao walikuwa kambini nchini Uturuki wataonekana mitaani kwa mara ya kwanza baada ya mechi ya Simba Day dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa.

 

Spoti Xtra limedokezwa kwamba viongozi wa Simba chini ya muwekezaji bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ wameamua vijana wafikie kwenye hoteli hiyo iliyoko katikati ya jiji ili kutuliza akili na kujiweka sawa kwa siku hiyo kubwa ya mashabiki wa Simba ambayo itakuwa ni sikukuu ya Nanenane Kitaifa.

 

Katika vyumba hivyo Simba watalazimika kutoa Sh. Milioni 18 kabla ya kuondoka na kuelekea Sea Scape ambapo wamekuwa wakiweka kambi mara kwa mara ambako nako pia ni ufukweni eneo la Mbezi.

 

Wachezaji wa Simba wamefurahia hali ya maisha inayoendelea ndani ya klabu hiyo na kusisitiza kwamba sasa ni muda wa kazi tu na mashabiki watafurahia sana msimu ujao.

STORI NA SWEETBERT LUKONGE | SPOTI XTRA

MASOUD AFUNGUKA

Mrundi Masoud Djuma ambaye ni Kocha Msaidizi wa Simba kutokana na maelewano yake mazuri na kocha wa wake mkuu, Mbelgiji, Patrick Assuems anaamini timu hiyo itafanya vyema msimu ujao.

 

“Kwa muda mfupi ambao nimekaa na huyu kocha tumekuwa tukishirikiana vizuri tu na kuelekeza pale ambapo pana kuwa tofauti na lengo na kujenga kikosi bora japokuwa kila mtu anakuwa na mfumo wake lakini yeye ndiye mkuu hivyo anasimamia vizuri.”

 

“Na kipindi hiki tunashirikiana vizuri sababu ndiyo tunajenga timu yetu na kuweza kutengeneza kombinesheni za wachezaji wetu hivyo lazima tuwe makini katika hilo sababu ndiyo nafasi ya pekee na tunahitaji kupambana kweli kuelekea kwenye msimu mpya.”

Comments are closed.