The House of Favourite Newspapers

Okwi: Mpaka Waombe Poo

Emannuel Okwi

STRAIKA namba moja wa Simba na mtupiaji tishio zaidi kwenye Ligi Kuu ya Bara msimu huu, Emannuel Okwi amesisitiza kwamba kwa uelewano walionao na pacha wake, John Bocco katika fowadi ya Simba mashabiki wavute pumzi.

 

Okwi ambaye alipotua Simba, mashabiki wa Yanga walikuwa wakimtania kuwa ni mhenga amesema uelewano mzuri kati yake na Bocco pamoja na morali waliyonayo ndiyo chachu ya kinachotokea Msimbazi kwa sasa na akasisitiza kuwa hawapoi mpaka kieleweke.

 

Okwi ambaye ni raia wa Uganda anayedaiwa kunyemelewa na klabu za Misri, kwa sasa ametimiza mabao 18 kwenye ligi akifuatiwa na Bocco mwenye mabao 13 ambapo wamepishana mabao nane.

Okwi anayemiliki miradi kadhaa nchini kwao ikiwemo biashara ya magari, amesema wanategemeana sana na Bocco ambaye ni nahodha na wanaingia kwenye kila mchezo wakiwa na lengo maalum la ushindi tu na timu nzima imehamasika.

 

Tuna maelewano mazuri na Bocco uwanjani kila mmoja anamtegemea mwenzie kwa kumtengenezea nafasi, Bocco ananitegemea mimi na mimi namtegemea lakini hata ikitokea mtu mwingine akija nafanya nae kazi haimaanishi kuwa yeye peke yake,” anasema Okwi huku akisisitiza kwamba Simba ya sasa ina ushirikiano mkubwa zaidi ya kipindi cha nyuma ndio maana hawakamatiki.

 

“Sina tageti yeyote niliyojiwekea ya kufunga mabao mangapi hadi mwisho wa msimu, ninachioangalia ni kuingia uwanjani kupambana kufunga kuisaidia timu yangu ili iweze kufanikiwa kufanya vizuri katika kila mchezo.

“Siku zote wajibu wangu ni kuingia uwanjani na kupambana na wenzangu, kuisaidia na kuitumikia timu yetu kuhakikisha tunapata ushindi katika kila mechi ili kupata matokeo mazuri ya pointi tatu zitakazotuweka katika nafasi nzuri zaidi,” anasema Okwi ambaye aliwahi kuichezea Yanga lakini hakung’ara.

 

Akizungumza Yanga na ubingwa Okwi anasema; “Bado huwezi kusema kwamba tumechukua ubingwa kwa sababu Yanga wanaweza kubadili upepo muda wowote ule na ili ujue umewapita basi hadi zibaki mechi tatu au mbili kabla ya ligi kumalizika.” “Ninatambua Yanga ni timu kubwa na ninaiheshimu hivyo kuwa mbele yao kwa tofauti ya pointi nane pekee hakuwezi kutufanya tubweteke kwani bado wana mchezo mkononi ili tulingane nao.”

 

Lakini Bocco anasema; “Sijajiwekea malengo ya namba ya mabao, ninachoangalia ni kuona nafanikiwa kufunga katika kila mechi. Ushindi wa Mbeya City umetupa matumaini sana.”

 

“Sasa tunaangalia mchezo wetu dhidi ya Prisons ambao tukishinda ndio utatupa nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa,” anasema mchezaji huyo wa zamani wa Azam ambaye awali alipopewa unahodha Simba baadhi ya mashabiki waling’aka baadae wakatulia.

 

Kocha Pierre Lechantre anasema; “Bocco na Okwi ndiyo bora kwa sasa kutokana na uwezo ambao wanauonyesha kwa kufunga mabao ambayo yamesaidia timu, nadhani utakuwa unajua ni kitu gani ninazungumzia wamekuwa na mchango mkubwa.”

 

REKODI

Katika rekodi za wafungaji bora wa Bara kwa misimu sita mfululizo, Okwi amefanikiwa kuvunja tatu na bado amesalia na kibarua cha kutibua rekodi mbili pekee.

Okwi amebakiza rekodi ya Bocco ya msimu wa mwaka 2011/12 ambayo alifunga mabao 19 na Amissi Tambwe alikuwa kinara msimu wa mwaka 2015/16 alifunga mabao 21 na msimu wa 2013/14 alifunga mabao 19.

 

Okwi amevunja rekodi ya msimu wa mwaka 2012/13 ya Kipre Tchetche mabao 17, msimu wa 2014/15 ya Simon Msuva 17 na msimu uliopita ya Msuva na Abdulrahman Mussa mabao 14.

Endapo Okwi atafanikiwa kufunga mabao 21 basi atakuwa amevunja rekodi ya misimu sita mfululizo kuweza kufunga mabao mengi zaidi tangu msimu wa mwaka 2011/12 mpaka sasa.

NA KHADIJA MNGWAI | SPOTI XTRA

Comments are closed.