The House of Favourite Newspapers

Okwi na Niyonzima Kumbe Lao Moja

Haruna Niyonzima

EMMANUEL Okwi amewaambia mashabiki wa Simba kwamba licha ya yeye kutokuwa sehemu ya kikosi kwa sasa katika michuano ya Mapinduzi lakini kwa jinsi alivyoona kwenye Azam TV hakuna ya kuwazuia kubeba ndoo. Okwi hatofautiani na Haruna Niyonzima ambae amepewa kazi pevu ya kujifua bichi Jijini Dar es Salaam lakini anaamini kuwa kombe litakwenda Simba kwavile sasa vijana wameamua kufanya kazi.

 

Okwi, mwenye mabao nane katika Ligi Kuu Bara, ameshindwa kuwa sehemu ya wachezaji wa Simba wanaoshiriki Mapinduzi kutokana na kubaki kwao Uganda ambako anaendelea na matibabu ya enka. Akizungumza na Spoti Xtra, Okwi ambaye anasherehekea siku yake ya kuzaliwa Desemba 25 kila mwaka, alisema; “Mimi sipo ndani ya timu kwa sasa lakini nikwambie tu kuwa bado sijaona timu ambayo inaweza kuisimamisha Simba.”

Emmanuel Okwi

“Nasema hivyo kwa sababu ukitazama wachezaji ambao wapo, wana viwango vya hali ya juu sana na uzoefu mkubwa wa kufanya vyema katika michuano hiyo, imani yangu ni kwamba Simba lazima wachukue ubingwa huo wa Mapinduzi hata kama sipo,” alisema Okwi.

 

NIYONZIMA YUKO BICHI

Kocha wa Simba, Masoud Djuma amemwambia Haruna Niyonzima asibanduke bichi kama anataka kuwa fiti na arudi kwenye kikosi chake. Niyonzima aliyetua Simba katika usajili wa dirisha kubwa kwa dau la milioni 115 akitokea Yanga, kwa sasa ameshindwa kuwa sehemu ya kikosi hicho cha Simba ambacho kinapigania ubingwa wa Mapinduzi ambayo inaendelea visiwani Zanzibar kutokana na majeruhi.

 

“Kwa sasa kocha Masoud Djuma amenipangia programu maalumu ya kwenda bichi na kufanya mazoezi huko tena nikiwa pekupeku kwa ajili ya kujiimarisha tatizo la nyayo ambalo linanisumbua na kunifanya niwe nje ya timu kule Zanzibar katika michuano ya Mapinduzi.

 

“Naamini hadi pale watakaporudi nitakuwa nimepona na kuwa tayari kucheza kwa mara nyingine, kama siyo kocha Djuma basi kwa sasa ningekuwa nacheza kwani watu wanaona kama siumwi vile lakini yeye ameliona hilo na kunipa muda huu wa kupumzika na kufanya mazoezi kwa ajili ya kurejea katika hali yangu ya zamani,” alisema Niyonzima.

Comments are closed.