Okwi: Njooni Uhuru Mkashangilie Bao

Emmanuel Okwi

KINARA wa mabao kwenye Lig Kuu Bara, Emmanuel Okwi raia wa Uganda amefunguka kuwa baada ya kumaliza majukumu ya timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’, kwa sasa anaelekeza hasira zake juu ya wapinzani wao, Mtibwa Sugar kwa kuhakikisha anaipelekea maumivu timu hiyo kwa kuifunga.

 

Okwi mwenye mabao sita kwenye ligi hadi sasa, Jumapili hii anatarajia kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Simba kukabiliana na Mtibwa Sugar kwenye muendelezo wa ligi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar.

 

Ikumbukwe mshambuliaji huyo amerejea nchini akitokea kwao Uganda ambapo alienda kuichezea The Cranes kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Ghana, mchezo uliomalizika kwa suluhu. Hata hivyo ndoto ya kikosi hicho kutinga kwenye fainali hizo zimeshapotea kutokana na wapinzani wao Misri kufuzu kutoka kundi lao.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Okwi amesema baada ya kuumaliza mchezo huo wa Uganda kwa sasa anaelekeza nguvu na akili zake kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kuhakikisha anaipa matokeo mazuri timu yake na jambo hilo linachangiwa na yeye kushindwa kuifungia bao lolote timu yake kwenye mechi mbili zilizopita.

 

“Tayari nimeshamaliza majukumu ya timu ya taifa, tulipambana kwa kiasi kikubwa na kila mtu aliona na sasa nimerejea tena Bongo kwenye kikosi changu kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo kwa upande wangu nipo fiti kabisa kuwamaliza.

 

“Nataka kufunga kwenye mchezo huu, kwa maana katika michezo yetu miwili iliyopita sikufunga bao lolote lile ingawa tulipata matokeo mazuri, nataka kuisaidia timu yangu ipate matokeo mazuri, kwa hiyo nitakuwa na kibarua cha kuibeba ili tupate pointi tatu,” alisema Okwi.

Stori: Said Ally na Musa Mateja

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment