The House of Favourite Newspapers

Omog Akutana Chemba Na Wachezaji 7 Simba

Aliyekuwa Kocha wa Simba, Joseph Omog.

JOSEPH Omog kabla ya kuondoka nchini juzi Ijumaa alikaa kikao cha dharura na wachezaji wa timu hiyo wakiongozwa na nahodha John Bocco na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kuwaachia ujumbe mzito.

 

Wachezaji wengine waliokutana na kocha huyo mapema kabla ya safari yao ya Mtwara ya kwenda kupambana na Ndanda FC katika mchezo wa ligi kuu uliofanyika jana ni Mghana James Kotei, Mrundi Laudit Mavugo, Jonas Mkude, Said Ndemla pamoja na Juma Luizio.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, mmoja wa wachezaji hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema; “Alitusisitiza kuwa tusivurugane kabisa katika kipindi hiki ambacho ligi inaelekea katika ushindani wa kweli lakini pia tusitumie muda mwingi kumfikiria yeye kuliko kuitumikia Simba ambayo inahitaji mafanikio kupitia sisi.”

 

“Pia alitutaka tushirikiane na kocha Masoud Djuma kama tulivyokuwa tukifanya kwake na amemtaka Bocco ambaye ni mzoefu wa kuongoza wachezaji wenzake ili tuweze kuwa kitu kimoja katika mbio hizi za kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu huu,” alisema mchezaji huyo.

 

Alipoulizwa Omog, kuhusiana na hilo alisema kuwa: “ Ni kweli nilikutana na wachezaji hao kabla ya kuondoka kwani ni vijana wangu niliyofanya nao kazi vizuri bila ya tatizo lolote na niliwashauri mambo mengi ambayo wanatakiwa kufanya kwa faida yao lakini pia Simba.”

 

Omog alikumbwa na balaa la kutimuliwa Simba hivi karibuni baada ya timu hiyo kutupwa nje ya michuano ya Kombe la FA na timu ya Green Warriors inayoshiriki Ligi Daraja la Pili.

 

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja Azam Complex, Simba ilifungwa kwa penalti 4-3.

STORI: SWEETBERT LUKONGE | SPOTI XTRA

Comments are closed.