The House of Favourite Newspapers

Omog apangua kikosi Simba SC

0

SIMBA DAY (2)Kikosi cha timu ya Simba.

Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge
USIIONE Simba imekuwa tamu ukadhani benchi la ufundi limeridhika! Katika kuhakikisha anatimiza ahadi yake ya kushinda kila mechi ya Ligi Kuu Bara, kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog, amekipangua kikosi chake kidogo kwa kuwaingiza na kuwaondoa wachezaji watatu kwenye ‘First Eleven’ yake.

Joseph-Marius-Omog

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog.

Mabadiliko hayo ya kikosi chake yanatarajiwa kuonekana kwenye mechi ya leo ya ligi kuu wakati timu hiyo itakapopambana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wanaotarajiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ni Mganda, Juuko Murshid akipishwa na Novalty Lufunga huku Fredric Blagnon raia wa Ivory Coast akimuondoa Ibrahim Ajib na Malika Ndeule akianza kuchukua nafasi ya Hamad Juma aliyetereza chooni na kupasuka kichwani.
Katika mazoezi ya siku mbili waliyoyafanya Simba kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran, Dar, Mcameroon huyo alionekana akipanga vikosi viwili huku kimoja akionekana akikipa maelekezo na mbinu mbalimbali za ndani ya uwanja.
Kikosi hicho alichokuwa anakipa maelekezo kocha huyo ambacho huenda kikaanza kwenye mechi ya leo dhidi ya JKT Ruvu kiliundwa na kipa, Vincent Angban, Malika Ndeule, Mohammed Hussein Zimbwe, Juuko, Method Mwanjale, Jonas Mkude, Jamal Mnyate, Mzamiru Yassin, Blagnon, Laudit Mavugo na Shiza Kichuya.
Wakati mazoezi hayo yanaendelea, washambuliaji Mavugo na Blagnon walionekana wakicheza kwa kuelewana huku wakitengenezeana nafasi za kufunga mabao.
Katika mazoezi hayo, Blagnon alionekana kuwavutia mashabiki wa timu hiyo waliofika kuangalia mazoezi baada ya bao lake safi la kichwa alilolifunga akiunganisha krosi ya Kichuya.
Mara baada ya mazoezi hayo kumalizika, kocha huyo alizungumza na Championi Jumamosi na kusema: “Wala usishangae kuona mchezaji aliyepo kwenye kikosi cha kwanza, kwenye mechi inayofuata akaanzia benchi.
“Kikosi changu nitaendelea kukiimarisha kila kukicha na kikubwa ninataka kuona kila mchezaji anaonyesha kiwango kizuri ndani ya uwanja pale anapopata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
“Kama mchezaji nikimpa nafasi ya kucheza na akashindwa kuitumia vema, basi mechi ijayo usitarajie kumuona akicheza, nitampa nafasi mwingine na kikubwa ninafurahia kuwa na kikosi kipana katika kikosi changu cha msimu huu,” alisema Omog.

Leave A Reply