The House of Favourite Newspapers

Oprah Winfrey anakufungia mwaka kwa somo la utajiri

a5f3a7aa4d4cb83571662286f3796327

Makala: Nyemo Chilongani na Mtandao | Gzeti la Ijumaa Wikienda, Toleo la Desemba 26, 2016

Si maneno yangu tu, hata mabilionea wenyewe husema kila siku kwamba, ili ufanikiwe katika maisha yako ni lazima upambane, ujinyime na ujitume huku wakati mwingine ukijinyima baadhi ya vitu ilimradi ufanikiwe.

Kupitia safu hii kwa mwaka mzima tuliwasikia mabilionea wengi, walifunguka namna ya kufanikiwa, vitu gani unatakiwa kufanya ili ufanikiwe na kutoka hapo ulipokuwa. Leo tunaona baadhi ya mambo ambayo yalimfanya bilionea, Mtangazaji na Mwigizaji wa Marekani, Oprah Winfrey kufanikiwa na hata yale ambayo huyafanya na kuendelea kuunenepesha utajiri wake.

Pamoja na kwamba, Oprah alipitia katika maisha ya kukata tamaa lakini alipambana. Wapo waliomrudisha nyuma, waliomwambia hawezi kufanikiwa kwa sababu ni mwanamke mweusi lakini hakutaka kuwasikiliza, hakutaka kuyaingiza maneno yao moyoni mwake.

Leo hii Oprah ni bilionea mkubwa, anaheshimika kila kona, utajiri wake wa dola bilioni 2.9 (zaidi ya trilioni 6) haukupatikana kwa kulala au kwa bahati tu. Ili kuupata, ilimbidi apambane sana, kujituma usiku na mchana.

Kupitia Oprah, haya ni baadhi ya mambo anayokuambia unapaswa kuyafahamu kabla na baada ya kuwa bilionea;

oprah-winfreyUSIAMINI KATIKA BAHATI

Katika mahojiano yake na vituo mbalimbali vya televisheni, Oprah anasema: “Katika kipindi ambacho sikuwa kama nilivyo, niliamini katika bahati, nilijisemea kwamba watu wote waliofanikiwa walikuwa na bahati, mimi sina bahati hivyo sikutakiwa kujisumbua.

“Baadaye nilikutana na watu waliofanikiwa, wakaniambia sikutakiwa kuamini katika bahati bali kupambana, hivyo nikapambana na kuwa hapa nilipo. Kwangu mimi bahati ni maandalizi, ili bahati ikufuate ni lazima ujiandae, bahati haiwezi kuwakuta watu wasiojiandaa.”

KILA MTU HUFANYA MAKOSA

Oprah anaendelea kwa kusema: “Hakuna binadamu aliyekamilika, kila mtu hufanya makosa. Nilikuwa na tabia chafu katika usichana wangu. Nilifanya makosa lakini sikutakiwa kuyarudia au kukaa na kujuta kwamba nilifanya makosa. Nilitakiwa kusahau pale ambapo nilianguka. Katika kipindi hiki nilitakiwa kusimama imara zaidi. Wengi wamekuwa hawafanikiwi kwa sababu ya makosa waliyoyafanya huko nyuma. Mtu atasema yeye alikuwa mlevi, alipoteza muda mwingi kunywa pombe hivyo hawezi kufanikiwa, mwingine atasema alikuwa mwizi, hivyo hawezi kufanikiwa. Ndugu yangu, kama mimi nilikuwa na tabia chafu na nikafanikiwa, vipi kuhusu wewe? Tunafanya makosa, sawa, ila yasituendeshe kila siku.

PAMBANA, FANYA KAZI KADIRI UWEZAVYO

“Ni lazima ujue kwamba mafanikio hayapatikani kwa watu wasiopambana. Ili ufanikiwe ni lazima upambane usiku na mchana, ndivyo nilivyofanya. Baada ya kufanikiwa, sikutaka kutulia kwa kusema kwamba imetosha nianze starehe, nilitakiwa kufanya kazi kwa bidii, nilijifunza kwa watu waliofanikiwa na mpaka kuwa hapa nilipokuwa.

“Unapotaka kufanikiwa, huna budi kujitoa kwani kama ufalme wa Mungu unapatikana kwa watu waupiganiao, basi hata utajiri unapatikana kwa watu wautafutao kwa bidii.

 

UNATAKIWA KUAMINI KATIKA MAFANIKIO

“Bibi yangu alikuwa mfanyakazi wa ndani, katika maisha yote ya utotoni, bibi alikuwa akiniambia kwamba na mimi nilitakiwa kujifunza kufua, kuanika nguo na kupika kwa sababu kuna siku nami nitakuwa mfanyakazi wa ndani.

“Yeye alikuwa akiamini hivyo ila moyoni mwangu sikuwahi kuamini kwamba kuna siku nitakuwa mfanyakazi wa ndani. kwa sababu nilijisemea hivyo kwa kuamini kwamba sikutakiwa kufanya kazi za ndani, kweli imani yangu ikanijenga, nikapambana huku nikisema kwamba sikutakiwa kuwa mfanyakazi wa ndani kama bibi yangu na hakika nimefanikiwa.

KUWA NA NJIA NYINGI ZA MAPATO

“Sikuzaliwa katika familia ya wafanyabiashara ila nilijifunza mambo mengi kutoka kwa wafanyabiashara wengi kama Bill Gates, Donald Trump, Familia ya Rockerfeller na wengine kwamba kamwe mtu hutakiwi kuwa na njia moja tu ya kuingiza mapato.

“Unatakiwa kuanzisha biashara nyingi,tofauti ambazo zitakufanya kukusanya fedha nyingi kila siku. Nimekuwa nikifanya hivyo, mbali na kuwa na kipindi changu cha televisheni lakini bado kuna biashara nyingine zinaniingizia fedha, hivyo na wewe unatakiwa kuiga kitu hicho kama nilivyoiga kwa watu walionitangulia.

KUWA NA MATUMIZI YA WASTANI

“Watu wengi wamekuwa hawafanikiwi kutokana na matumizi yao makubwa. Mbaya zaidi, wengine baada ya kufanikiwa, wamekuwa wakifilisika kutokana na utumiaji mkubwa wa fedha zao. Kama mfanyabiashara anayeendelea kutafuta fedha, hutakiwi kuwa na matumizi makubwa. Itashangaza kuona ukiwa na matumizi makubwa kuliko kiasi unachokiingiza. Ni lazima uwe na nidhamu ya fedha, ukifanikiwa katika hilo, hakika utafanikiwa katika maishani yako.”

ILIKUPITA HII?

Mpaka Home; Haya Ndo’ Maisha Halisi ya Darassa, Cheki Video Akipika Msosi Gheto

Comments are closed.