P-Funk Hataki Kumsikia Mtu Zaidi ya Rapcha

NGULI kwenye muziki wa Bongo Fleva, P-Funk Majani amefunguka kuwa, kwa sasa nguvu na akili yake imeegemea katika upande wa rapa mpya kwenye tasnia hiyo Rapcha na hataki kuwaza msanii mwingine kwa sasa.
P-Funk ambaye ni mtayarishaji na mmiliki wa Studio ya Bongo Records aliyasema hayo alipofanya mahojiano na +255Global Radio kwenye kipindi cha Bongo 255 kinachoruka Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 10:00 jioni.
P-Funk alisema Rapcha ni msanii ambaye ameonyesha kuwa na kitu cha tofauti kwenye gemu, hivyo ameamua kuwekeza nguvu zake kwake ili aweze kuyafikia malengo yake na kuongeza kuwa hatoacha kumshika mkono dogo huyo kutoka Shinyanga hadi aweze kuwa msanii mkubwa Bongo.
“Kwa sasa nguvu yangu ipo kwa Rapcha tu, wala siwazi wasanii wengine, huyo dogo ana kitu cha tofauti ambacho kwa muda mrefu tumekimisi kwenye gemu. Hivyo, mimi nitafanya kila kitu kuhakikisha anafika mbali, akifika kule ndipo nitaanza kuwatazama wasanii wengine,” alisema Majani.

Majani prodyuza ambaye ana rekodi ya kutengeneza kazi nyingi na kubwa zilizoibadilisha ramani ya Bongo Fleva, akifanya kazi zilizobeba umaarufu mkubwa zikiwemo Starehe ya Ferooz, Zali la Mentali ya Professor Jay, Hakuna Kulala ya Juma Nature na nyingine nyingi za marehemu Ngwair, Fid Q na Dully Sykes.
Rapcha ni rapa mpya kwenye gemu ambaye ujio wake umewashitua watu wengi, ambapo kwa sasa yupo mjini kupitia wimbo wake wa Amen akiwa amemshirikisha Lady Jaydee. Wimbo huo ulitoka Julai 17 na hadi sasa umetazamwa zaidi ya mara 135,000 katika mtandao wa YouTube.
Issa Liponda, Dar es Salaam

