The House of Favourite Newspapers

‘PAKA MTU’ AZUA TAHARUKI

GEITA: Sintofahamu na taharuki imewakumba wakazi wa Kitongoji cha Buseresere, wilayani Chato mkoani Geita kufuatia mnyama anayetajwa kama paka mtu kuleta mauzauza; Amani limedokezwa. 

 

Usiku wa hivi karibuni inadaiwa kuwa paka mtu huyo liyekuwa amefungwa hirizi nyeusi shingoni aliingia kimiujiza nyumbani kwa Abdalah Hassani na kuanza kulia milio ya ajabuajabu.

Kulikonikulikoni iliyoambatana na hofu iliwakumba wenyeji wa nyumba hiyo ambapo walitoka na kumshuhudia paka huyo akiwakodolea macho na kuwafanyia mambo ambayo hawakuyaelewa. “Ikabidi nianze kukabiliana naye kwa kumpiga, baadhi ya majirani wakaja, cha ajabu wakati tunampiga akawa analia kama mtu.

 

“Hilo halikututisha, baada ya kumpiga kwa muda mrefu akafa, lakini baadhi ya watu wakasema tumkate kichwa kwa sababu anaonekana si paka wa kawaida na kwamba tukimwacha bila kumfanyia hivyo uhai utamrejea,” alisema Abdallah.

 

Aliongeza kuwa baada ya kukubaliana kufanya hivyo zoezi la kumkata kichwa lilifanyika ambapo baadaye mzoga wake waliutoa ndani ya nyumba hivyo na kwenda kuutupa jalalani wakisubiri kuche ili wamzike kabisa.

 

Mambo yote hayo yalifanyika bila kuwa na gumzo kubwa mtaani, lakini siku iliyofuata habari ya paka ikawa kinywani mwa kila mkazi kutokana na madai kwamba mnyama huyo aliyekatwa kichwa alikutwa akiwa amekiunganisha kama kawaida.

 

“Nilipoamka asubuhi kwenda kwa yule paka nikakuta ana kichwa chake kama jana yake, nikashangaa, ikabidi jirani tuliokuwa nao jana usiku nao waje kujionea tukio hilo,” alisema Abdallah.

Aidha, baada ya madai hayo, Amani lilimuuliza mtoa habari anathibitishaje kuwa mnyama huyo walimkata na kwamba kichwa chake kimejiunga kimazingaombwe ambapo alisema: “Unaona hizi damu (alionesha eneo lililokuwa limetapakaa damu) tulimkatia kichwa hapa; watu wote waliokuwepo walishuhudia.

 

“Ndiyo maana kila mtu anashangaa,” alisema na kuongeza kuwa kwa takriban wiki mbili nyumba yake imekuwa ikikumbwa na matukio ya mauzauza jambo ambalo alisema huenda kuna ushirikina anafanyiwa. Kufuatia madai hayo, Amani lilimtafuta mwenyekiti wa kitongoji hicho, Michael Chasama ili kujua paka anawezaje kukatwa kichwa na kisha kikajiunga tena?

 

“Hapa kumekuwa na imani za kishirikina ndiyo maana unaona taharuki inatokea miongoni mwa jamii, lakini mimi nawaomba wakazi wa eneo hili wapuuze imani hizi potofu,” alisema mwenyekiti huyo. Katika kutokomeza imani hizo za kishirikiana upo mpango wa kuwashirikisha viongozi wote wa dini ili wafanye dua na maombi ikiwepo kuwaelimisha waumini wao kuepukana na mambo ya kishirikina.

Amani lilibaini kuwa wakazi wengi wa kitongoji hicho wanaamini mambo ya ushirikina ambapo hata kwenye tukio hilo la paka anayetajwa kuwa na tabia kama binadamu walidai kuwa wakati watu wakimpiga kuna nyumba ya jirani alisikika mtu akiugulia maumivu kana kwamba alikuwa akipigwa yeye.

 

Hata hivyo akili ya kisayansi haipati jibu paka anawezaje kujiunganisha kichwa mwenyewe halafu aendelee kufa kama alivyokutwa na watu siku ya pili yake.

 

Wito wa Amani kwa viongozi wa serikali na dini wa eneo husika ni kuitokomeza imani hiyo ya kishirikina miongoni mwa jamii kwani imekuwa ikisababisha madhara makubwa yakiwemo mauaji jambo ambalo serikali imekuwa ikilikemea kwa nguvu zote.

 

Filamu ya paka huyo kudaiwa kujiunganisha kichwa alichokatwa na binadamu iliishia kwa wakazi wa eneo hilo kuutwaa mzoga wake na kwenda kuuchimbia ardhini mbali na makazi ya watu.

BREAKING: Viongozi Wa CHADEMA Watoa Tamko ZITO!

Comments are closed.