The House of Favourite Newspapers

Pambano la Anthony Joshua vs Wladimir Klitschko ni leo Usiku

0
Anthony Joshua wa Uingereza (kushoto) na Wladimir Klitschko wa Ukraine wakipima uzito kuelekea pambano lao la leo usiku.

MABONDIA Anthony Joshua wa Uingereza na Wladimir Klitschko wa Ukraine leo Jumamosi usiku wanapigana kwenye Uwanja wa Wembley kuwania mataji ya IBF, WBA na IBO katika uzito wa juu.
Joshua ni bingwa mtetezi wa taji la IBF wakati mataji WBA na IBO yanawaniwa bila ya kuwa na mtetezi. Pambano hili linachezwa likitajwa kubwa kuchezwa Uingereza katika miaka ya hivi karibuni.

Anthony Joshua akijiweka sawa kabla ya pambano.

Hili ni pambano la pili kubwa la ngumi kuchezwa kwenye uwanja huo baada ya lile la Carl Froch na George Groves lililopigwa Mei 2014. Gumzo kubwa katika pambano hili ni historia za mabondia hao.

Wladimir Klitschko wa Ukraine kabla ya pambano.

Promota Eddie Hearn alitangaza Januari mwaka huu kwamba, tiketi 80,000 zilikuwa zimeshauzwa na huku zikitarajiwa kufikia 90,000 na kuvunja rekodi ya pambano la Froch na Groves.
Meya wa London, Sadiq Khan amesisitiza kwamba, pambano hilo linavunja rekodi ya mwaka 1939 wakati Len Harvey na Jock McAvoy walipopambana.

Joshua akichat na mashabiki wake.

HISTORIA
Pambano hili linachezwa baada ya pambano la Klitschko na Tyson Fury kuhairishwa kutokana na Fury kupata matatizo ya kiafya. Ikumbukwe Fury alikuwa akishikilia mikanda ya WBA na IBO.
Ilikuwa lazima Klitschko apambane tangu alipopigwa na Fury Novemba 28, 2015, lakini tatizo lilikuwa katika jinsi ya kuunganisha mataji hadi hivi karibuni WBA na IBO walipokubali kutoa mataji yao.


Fury alivuliwa mataji hayo ya WBA na WBO baada ya kushindwa kuyatetea katika muda muafaka pia kushindwa kupigana na Klitschko ndani ya wakati uliotakiwa. Ndipo Hearn alipotengeneza pambano hili.
Pambano hili linatajwa kwa na thamani ya dola milioni 53 sawa na Sh bilioni 117.


ANTHONY JOSHUA
Joshua ana umri wa miaka 27 tu lakini anaonekana ni miongoni mwa mabondia hatari katika uzito wa juu kwani hadi sasa amepigana mapambano 18 na kushinda yote, tena kwa Knock Out yaani ‘KO’.



Jina la utani la Joshua ni ‘AJ’, ana urefu wa futi 6 na inchi 6 na anapigana kwa mtindo wa Orthodox, na ameweka mezani mkanda wake wa IBF alioutetea Desemba 10, mwaka jana baada ya kumtwanga Éric Molina.
Katika pambano hili, Joshua ataingiza pauni milioni 15 ambazo ni sawa na Sh bilioni 42.4, vyovyote itakavyokuwa yaani akipigwa, akishinda au akitoka sare.
“Mwanzo Klitschko aliniita mdogo wake, lakini sasa ananiita mpinzani wake anasema sina kitu ila misuli minene, naamini nina nafasi ya kushindi kwani napigana na mzoefu,” anasema Joshua.

WLADIMIR KLITSCHKO
Wladimir Klitschko ni mbabe kutoka Kiev, Ukraine ambaye aka yake ni ‘Dr. Steelhammer’. Klitschko ana rekodi ya kupigana mapambano 64, ambapo amepoteza manne. Ameshinda mara 60 kati ya hizo, 53 ni KO.
Kama ilivyo kwa Joshua, Klitschko ana urefu wa futi 6 inchi 6, anapigana kwa mtindo wa Orthodox. Huyu na umri wa miaka 41.


Katika pambano hili, Klitschko anatarajiwa kupata kiasi cha fedha ambacho hakitaweza kumzidi Joshua anayeweka mezani taji lake.
“Kipigo cha Fury kimeniamsha na kutakiwa niwe tayari muda wote, sitajali umri au misuli ya mtu ninayepambana naye, najua nina changamoto lakini nimejipanga kushinda pambano hili,” anasema Klitschko.

MAPAMBANO MENGINE
Kabla ya pambano la Joshua na Klitschko, mapambano kadhaa ya utangulizi yatapigwa ambapo Scott Quigg atapigana na Viorel Simion katika uzito wa unyoya huku Luke Campbell akipigana na Darleys Pérez kwenye uzito wa kati.
Kwa wanawake, Katie Taylor atapigana katika uzito wa kati na Nina Meinke wakati Lawrence Okolie atazichapa na Russ Henshaw na Josh Kelly atapambana na Faheem Khan.

Leave A Reply