The House of Favourite Newspapers

Pamoja na Changamoto zake, Treni Ya Mwendokasi, Gen Z Wanapaswa Kulijua Gari Moshi Hili – Video

0

Rais Samia Suluhu Hassan, Agosti 1, 2024 alizindua rasmi safari za treni ya umeme, Standard Gauge railway, kwa kifupi wanaita SGR kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Morogoro mpaka Dodoma, ikiwa ni mafanikio makubwa ya mradi huo wa kimkakati ambao sasa unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika, kuwa na reli na treni za kisasa za kiwango cha SGR.

Waswahili wanasema ada ya mja ni kunena, uungwana ni vitendo. Tangu ujenzi wa reli hiyo ya kisasa ulipoanza April, 2017 kwa kipande cha Dar es Salaam- Morogoro, waja walinena. Wapo walionena kwa mema, lakini wapo pia waliobeza na kutoa maneno ya kukatisha tamaa kuhusu mradi huo.

Hayawi hayawi sasa yamekuwa, kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kwa muda mfupi zaidi kuliko hata mabasi, hatimaye siyo ndoto tena! Ni jambo ambalo sasa linawezekana, unaenda zako stesheni, unakata tiketi na unateleza kama Ulaya mpaka Dodoma.

Bado baadhi ya waja hawajaacha kunena kama ilivyo ada yao! Hitilafu kidogo tu kwenye treni za SGR inakuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii, kila mtu anasema lake.

Hivi nyie waja, hasa kizazi hiki cha sasa, mnaita Generation Z au Gen Z, mnaijua historia ya usafiri wa treni kweli? Mnajua ni magumu kiasi gani taifa limepitia mpaka leo usafiri wa treni unaonekana kuwa luxury kuliko hata mabasi?

Kama ulikuwa hujui, usafiri wa treni nchini una safari ndefu, tangu enzi za mkoloni huko. Unalijua gari moshi wewe? Unaambiwa enzi hizo usafiri wa treni ilikuwa ni zaidi ya mateso.

Treni za mwanzo zilikuwa zikiendeshwa kwa injini zinazofua umeme kwa kutumia makaa ya mawe. Ukisikia gari moshi, ndiyo haya sasa ya tangu enzi za mkoloni. Treni likiwa linatembea, moshi unaotoka kwenye injini ni zaidi ya moshi wa tanuri la kuni mbichi.

Leave A Reply