PanAfrican Energy Tanzania Yatoa Mitungi 500 ya Gesi Kuchangia Nishati Safi ya Kupikia
Dar es Salaam, 14 July 2024 – Katika hatua kubwa ya kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia, kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET) inafurahi kutangaza mchango wa mitungi 500 ya gesi ya kupikia Pamoja na vichwa vyake.
Mpango huu ni sehemu ya mkakati wa taifa kujenga matumizi ya mifumo safi, salama na bora ya kupikia. Mchango huu utagawanywa katika mikoa ya Mara, mitungi 200 na mitungi mia kwa mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Dodoma. Kila mkoa ukipatiwa mitungi 100.
Ikiwa na historia ya miaka 20 ya shughuli za gesi katika kisiwa cha SongoSongo, PAET imedhamiria kutoa nishati salama, safi, inayotegemeka kwa matumizi ya kuzalisha umeme, matumizi ya viwandani, usafiri na masoko mengine. Kampuni imejikita kuhakikisha kuwa athari zitokanazo na shughuli zake kwa mazingira ni madogo iwezekanavyo na kuwa na nafasi muhimu katika mkakati wa Tanzania kuwa na uchumi msafi zaidi.
Mitungi hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa Mbunge Janeth Masaburi mbele ya Naibu Waziri, Ofisi ya makamu wa Rais (Mazingira), Mhe. Hamisi Hamza Chillo aliyemuwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe Dotto Biteko. Akizungumza katika shughuli hiyo, Waziri huyo alisema; “Tunamshukuru mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya kuhakikisha tunatumia nishati safi, pia amekuwa kinara barani Afrika kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, nimpongeze pia mheshimi wa Janeth Masaburi kuja na mpango huu mkoani Dar es Salam ili kumtua mama kuni kichwani”
Mhe. Masaburi pia alieleza furaha yake kwa mchango huo akisema; “Kipekee nipende kumshukuru mheshimiwa Rais kwa mpango huu wa nishati safi ya kupikia ili watu waondokane na vifo vitokanavyo na nishati chafu, kauli mbiu yetu ni “ Masizi TupaKule” Rais alikuja na mpango huu ili kumtua mama kuni kwa matumizi ya nishati mbadala ya kupikia.
Na mimi nimeamua kumsaidia kwa kutoa hamasa kwa jamii hususani kwa wakinamama waweze kutumia nishati safi waachane na matumizi ya kuni na mkaa. Alisema Mhe. Masaburi. Aliongeza kusema; “Nipende kutoa shukurani zangu za dhati kabisa kwa wafadhili wetu wakiwemo mfadhili mkuu Stamico na wengine wakiwemo PanAfrican Energy Tanzania ambao wameweza kutushika mkono kuhakisha tunafanikisha suala letu.”
Kuendana na mpango wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia uliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, PAET inaona mchango huu kuwa kielelezo cha dhamira yake kuboresha maisha yaWatanzania. Kwa kuchangia nishati safi ya kupikia, PAET inasaidia matokeo chanya ya afya na mazingira katika jamii.
Zaidi ya kuchangia kampeni ya taifa ya nishati safi ya kupikia, PAET imekuwa ikiwekeza kwa miaka kadhaa katika miradi tofauti katika kisiwa cha Songosongo na wilayani Kilwa. Miradi hii ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa kwenye sekta za elimu na afya inaendana na dhamira ya PAET kuboresha hali za jamii zinazoizunguka.
Meneja wa Uwajibikaji kwa Jamii wa PAET, Andrew Kashangaki alisema; “tuna furaha kubwa kuchangia mkakati huu wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia na kuchangia kuboresha hali za jamii za Kitanzania. Tunaichukia kuwa wajibu wetu kusaidia mipango ya serikali na Wizara ya Nishati katika jambo hili.”
Mitungi hiyo na vichwa vitagawiwa kwa makundi kadhaa nchini ambao wako hatarini zaidi kutokana na matumizi ya nishati isiyo salama.