The House of Favourite Newspapers

Panga Kali Kuwafyeka Wanaojipitisha Majimboni!

0

DAR: Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitarajia kufungua pazia kwa makada wake kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa nafasi za ubunge na udiwani kuanzia Julai 14 hadi 17, mwaka huu, baadhi yao tayari wameanza kujipitisha na kutangaza nia kinyume na kanuni za uchaguzi za chama hicho, IJUMAA linaripoti.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya makada wanaotarajia kuwania kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge na udiwani, kuanza kutangaza nia kwenye vyombo vya habari na wengine kutengeneza makaratasi, vipeperushi vya kampeni vinavyoshawishi na kuvisambaza katika mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, Facebook na Twitter.

 

Aidha, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi CCM zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2017, zimebainisha kuwa mienendo hiyo ya makada hao ni kinyume cha taratibu za uchaguzi.

 

Kanuni hizo zimebainisha wazi suala hilo katika kifungu cha 35 (16) kinachosema; “Ni marufuku kwa mgombea wa ngazi yoyote kuzunguka matawini, katani, wilayani na mikoani kukutana na wajumbe wa mkutano utakaomchagua kwa kisingizio cha kujitambulisha, kuwasalimu wajumbe au kuwapa nauli. Mgombea atakayethibitika anazunguka, ataondolewa katika orodha ya wagombea.”

 

Pia kanuni ya 35 (12) nayo imeelekeza kuwa; “Ni mwiko kutumia makaratasi ya kampeni nje ya utaratibu wa chama au kutumia vishawishi vya aina yoyote kwa minajili ya kupata kura.”

 

Akifafanua kuhusu kanuni hizo, mmoja wa mawakili maarufu nchini, Bashir Yakub alisema kanuni hizo zimebainisha wazi kuwa, watia nia wengi waliotengeneza makaratasi na vipeperushi vya kampeni, wamekwenda nje ya utaratibu.

 

“Kwa sababu wengine wamethubutu hata kuomba kura kwenye vipeperushi hivyo, achilia mbali wale wanaovitumia kunadi sera za nini watafanya. Ni hatari.

“Watu wamepagawa kama vile chama hakina taratibu za kampeni na uchaguzi. Heri yao waliokaa kimya, huwenda hili likawa neema kwao,” alisema.

 

Alisema kwa kuwa CCM ni chama ambacho kinajitanabaisha kulinda nidhamu, utangamano, miiko, maadili na kanuni, kitajielekeza katika kanuni ya 36 kushughulika na watu wa namna hiyo.

 

“Kwa sababu kanuni imesema hivi, ‘Kiongozi au mwanachama yeyote atayethibitika kuwa amevunja kifungu chochote cha miiko hii, atadhibitiwa. Ikibidi atanyang’anywa ushindi alioupata na kukatazwa kugombea uongozi kwa muda utakaowekwa’.

 

POLEPOLE: TUTAWASHUGHULIKIA

Aidha, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole alisema makada hao waliovunja kanuni hizo, wataanza kushughulikiwa ndani ya vikao vya chama.

“Hao tutaanza kushughulika nao muda si mrefu, wewe subiri kuanzia tarehe 14 mpaka 17 kwenye mchujo, ndipo watakaposhughulikiwa,” alisema.

 

DIALLO: WENGI HAWAJUI KANUNI

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Dk Anthony Diallo, alisema licha ya kanuni hizo kukataza, imedhihirika kuwa wanachama wengi hawazijui.

“Ndiyo, ni makosa wanayofanya, ila saa nyingine viongozi tunawahurumia kwa sababu bahati mbaya kanuni za chama mpaka uzisome wakati nakala siyo nyingi kiasi cha kuwafikia kila mmoja.

 

“Wengine wanafuata kanuni zile walizotumia kugombea uchaguzi mkuu uliopita wakidhani kanuni ni zilezile,” alisema.

Alisema licha ya kwamba ni kanuni ambazo zinalenga kutoa mwongozo kwenye chaguzi ili ufanyike kwa amani, bado kanuni hizo hazijafahamika vema kwa makada wake.

 

Aidha, Diallo alionesha wasiwasi kuhusu kanuni hizo mpya na kubainisha wazi kuwa ni ngumu kutekelezeka.

“Kwa sababu hebu fikiria, upo kwenye mkutano wa kupiga kura, uonekane mara ya kwanza wakati wa kupiga kura, wajumbe watakuchagua kwa maelezo tu kweli! Lazima wakuelewe, sasa watu watakuelewaje kama haujipitishi kwao?” Alihoji.

 

Aidha, Dialo alikwenda mbali zaidi na kutoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na wagombea watakaojitokeza kutaka kuwania ubunge.

Alisema wananchi wanatakiwa kutoa kipaumbele kwa wagombea ambao ni wakazi wa maeneo yao ili waweze kutatua matatizo yao sawasawa pindi watakapochaguliwa.

 

“Kwa mfano, kanuni pia inasema Mtanzania anaweza kugombea popote, kwa sababu mama ni mzaliwa wa Mwanza, kada anatokea Lindi anapoishi anakuja kugombea Mwanza kwa sababu tu mama ni mzaliwa wa Mwanza, hilo ni tatizo.

 

“Tumewaambia kwamba wawe waangalifu, maana watakuja kulialia wakati matatizo yao hayajashughulikiwa,” alisema.

Baadhi ya makada wa CCM wanaotajwa kutangaza nia kwenye mitandao ya kijamii ni pamoja na Kitila Mkumbo (Kibamba), Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ (Iringa-Mjini) na Mchungaji Josephat Gwajima.

Stori: Gabriel Mushi, Ijumaa

Leave A Reply