The House of Favourite Newspapers

Panga La Mafaza Laja Yanga

Kikosi cha timu ya Yanga.

PANGA kubwa ambalo litaondoka na mafaza kadhaa linakuja ndani ya Yanga, hii inatokana na mabadiliko makubwa yaliyoonyeshwa na wachezaji vijana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi. Habari za ndani ya Yanga zinasema kwamba benchi la ufundi linafikiria kufanya hivyo mwishoni mwa msimu huu ili kuongeza ufanisi pamoja na kubadilisha aina ya uchezaji wa Yanga, ambao kwa kipindi kirefu ulikuwa unategemea wachezaji wakongwe wa ndani na nje ya nchi.

 

Miongoni mwa wachezaji hao wakongwe wamekuwa mzigo kutokana na kusumbuliwa na majeruhi kwa kipindi kirefu huku wakiwa wanaigharimu klabu. Miongoni mwa mafaza wanaotajwa ni pamoja na Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Nadir Haroub Canavaro na Amisi Tambwe.

 

VIJANA WAFUNIKA MAPINDUZI

Katika michuano ya Mapinduzi iliyomalizika jana usiku, Yohana Nkomola, ambaye alisajiliwa na Yanga katika kipindi cha dirisha dogo msimu huu akitokea kikosi cha Taifa ya Vijana Serengeti Boys ni miongoni mwa vijana waliotamba pamoja na Ramadhani Kambwili na Said Musa.
Nkomola ametamka kuwa baada ya mwaka mmoja Jangwani itatisha kwa sababu itakuwa na kikosi cha vijana ambacho kitakuwa na ushindani mkubwa, huku kocha wake Shadrack Nsajigwa naye akikiri hilo.

 

“Mimi kama mmoja wa wachezaji vijana ninaamini baada ya mwaka mmoja tutaweza kuifanyia Yanga mambo makubwa zaidi, mashabiki wetu wazidi kutusapoti ilikuweza kufanya vyema zaidi. “Tunashukuru kocha wetu ametupa nafasi kwenye Mapinduzi na vijana tumeweza kuonekana na sisi tutapambana hatutamuangusha tutazidi kupambana na kuwa bora,” alisema Nkomola. Hata hivyo, Nsajigwa ambaye aliwanoa wachezaji hao kuanzia kwenye timu ya vijana, alisema kiwango kilichoonyesha na wachezaji wote chipukizi kwenye Mapinduzi ni ishara kuwa wakiongeza juhudi watakuwa matata sana siku zijazo na wataibadili sura ya Yanga.

 

“Wachezaji chipukizi wamejitahidi kuonyesha uwezo na ilikuwa ni nafasi yao ya kucheza kwani tulitumia michuano hiyo kama sehemu ya mazoezi ya kujiandaa na ligi pamoja na michuano ya kimataifa. “Tunashukuru kuona kila mmoja ameonyesha kiwango cha juu hata wale ambao walikuwa hawapati nafasi ya kucheza walifanya vyema, hivyo inatupa nafasi ya kuamini kuwa tunaweza kufanya vyema zaidi,” alisema Nsajigwa.

MARTHA MBOMA,

Comments are closed.