The House of Favourite Newspapers

Pape N’daw mchawi

0

ABDOULAYE N'DAW PAPE

Mshambuliaji wa Simba, Pape N’daw.

KWA mujibu wa kamusi kadhaa za Kiswahili, neno ‘uchawi’ ni ufundi wa kutumia dawa au vitabu maalum vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe wengine’, pia inaweza kumaanisha ‘vifaa vinavyotumika kurogea’, kwa maana hiyo mchawi ni yule ambaye anahusika kufanya yote hayo.

Mshambuliaji wa Simba, Pape N’daw, juzi alizua sekeseke kwenye mechi ya timu yake dhidi ya Tanzania Prisons, ambapo wachezaji wa Prisons na mashabiki wengine wa mkoani hapa walijikuta wakitamka kuwa ‘huyu N’daw ni mchawi’.

Kauli hiyo ilitokana na kukutwa na kile kilichodaiwa kuwa ni hirizi wakati wa mchezo huo kwenye Uwanja wa Sokoine ambapo ilikuwa mara yake ya kwanza kuanza katika kikosi cha kwanza cha Simba, tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu.

Ilikuwa kama filamu, wakati mchezo ukiendelea, wachezaji kadhaa wa Prisons walikuwa wakimzonga mchezaji huyo, wakawa kama wanamuwinda vile, dakika ya 20, beki wa Prisons, Jumanne Efadhili, ndiye aliyejitoa mhanga na kuanza kudai kuwa ‘tall’ huyo wa Simba alikuwa na hirizi.

Kitendo cha kushikwa kiunoni na kutaka kufunuliwa ili waone hicho kilichodhaniwa kuwa ni hirizi kilisababisha msuguano mkubwa, wachezaji wa Simba walionekana kuingilia na kumtetea mwenzao huku wakipambana na wale wa Prisons.

Wakati zogo likiendelea kuwa kubwa, ndipo jezi ikafunuliwa na ‘mzigo’ huo ambao watoto wa mjini wanapenda kuuita ‘power bank’ yaani kiongeza chaji, ukaonekana na kusababisha mshtuko hata kwa wale wenzake wa Simba ambao baadhi yao wakaacha kumsaidia na kubaki wanatazama kinachoendelea kama filamu.

Kuona hivyo, wachezaji wa Prisons wakaendelea kumvaa wakimtaka aivue, ilibidi mwamuzi wa kati, Jimmy Fanuel alingilie na baada ya yeye kuiona power bank ikabidi amwamuru aende akaivue katika vyumba vya kubadilishia nguo.

Kuona hivyo, N’daw akawa mdogo na kwenda vyumbani kufanya yake, alirejea baada ya sekunde kadhaa kisha kuruhusiwa kuendelea na mchezo.

Wakati akielekea ndani ya vyumba hivyo, wale waliokuwa wamekaa kwenye benchi la Simba walionekana kutoamini kile wanachokiona na kujikuta wakiwa wameshika viuno tu.

Baada ya tukio hilo, mashabiki wa Simba ambao walikuwepo uwanjani hapo, uzalendo ukawashinda na kujikuta wakimzomea mchezaji wao kila alipopoteza mpira.
N’daw ambaye ni raia wa Senegal, alikuwa hapati nafasi, hivyo mchezo wa juzi ilionekana kama ndiyo siku ya kuanza kuonyesha makali yake, lakini kitendo cha kuingia na power bank na kisha kushtukiwa kinaweza kuwa kilizidisha kumvuruga na kushindwa kuisaidia timu yake ambayo iliishia kupata kipigo cha bao 1-0.
Aplina Philipo, Derick Lwasye na Musa Mateja, Mbeya

Leave A Reply