Pedeshee Ndama Apandishwa Kizimbani Tena

MFANYABIASHARA Ndama Hussein maarufu kama’Pedeshee Ndama’ na mwenzake Yusuph Hassan wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la kujipatia Dola 150, 000 kwa njia ya udanganyifu.
Kwa pamoja washtakiwa hao wamesomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Godfrey Isaya.
Wakili wa serikali Mwandamizi Christofa Msigwa, akisaidiana na Wakyo Simon wamedai kuwa mnamo Januari 21 mwaka 2020 washitakiwa hao kwa njia ya udanganyifu, waligushi nyaraka/risiti ya kuhifadhi kwa lengo la kudanganya kuwa Kampuni ya Lockfort Security Company Limited imepokea kilo 100 za dhahabu kutoka kwa Samuel Kabula wakati wakijua si kweli.
Aidha imeelezwa kuwa Machi 5, 2020, katika mkoa wa Dar es Salaam, washitakiwa hao pia waligushi mkataba wa mauziano kati ya Cozac Logiatics International Company Limited ya Tanzania na Innovative Perspective Company Limited ya Botswana kwa lengo la kuonesha kuwa Kampuni ya Cozac Logiatics International Company Limited imeingia mkataba wa kuuza dhahabu kilo 500 kwa kampuni ya Innovative Perspective Company (PTY) Limited kwa gharama ya dola 27,000 kwa kila kilo wakati wakijua si kweli.
Katika shitaka la utakatishaji fedha, imedaiwa kuwa kati ya Januari mosi 2020 na Februari 12 2021 washitakiwa hao walitakatisha Dola 150,000 wakati wakijua zilitokana na kosa tangulizi la kugushi.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo upande wa mashitaka umedai upelelezi wa kesi hi. yo bado haujakamlika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ambapo kesi imepangwa Machi 18 mwaka huu.
Washitakiwa wote wamepelekwa rumande kwakuwa kosa la utakatishaji fedha halina dhamana.

